Aliyemuua dada yake ahukumiwa kunyongwa

Thursday May 16 2019

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Moshi. Mkazi wa kijiji cha Tela Magula Wilaya ya Moshi, Modest Shayo (32) aliyemuua dada yake, Yasinta Ladislaus akimtuhumu kuingilia familia yake amehukumiwa kunyongwa.

Jaji Patricia Fikirini wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi ametoa hukumu hiyo leo Alhamisi Mei 16,  akisema mshitakiwa alikuwa na uwezo wa  kuzuia hasira yake kuepusha mauaji hayo jambo ambalo hakufanya.

Katika hati ya mashitaka iliyosomwa na mawakili wa Serikali, Akisa Mhando na Grace Kabu ilidaiwa kuwa, Februari 14, 2017 katika kijiji cha Tela Magula, mshtakiwa alimuua dada yake, Yasinta kwa makusudi.

Katika utetezi wake, mshitakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na mawakili Patricia Eric na Lilian Mushi alikubali kutenda kosa hilo kutokana na ugomvi wa muda mrefu na dada yake.

Katika hukumu yake, Jaji Fikirini alisema ameangalia utetezi wa mshitakiwa na kuona sababu ya kutenda kosa hilo haina mashiko kwani ugomvi alioueleza ulikuwa wa kawaida katika familia.


Advertisement