Lugola: Uchunguzi wa polisi umebaini video inayodaiwa ni ya Gwajima imetengenezwa

Thursday May 16 2019

Lugola, Uchunguzi ,Tanzanian ,pastor’s ,sex ,video , fabricated, Home, Affairs ,minister,  polisi, umebaini ,video , inayodaiwa , Gwajima, imetengenezwa

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Tanzania, Josephat Gwajima  

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amesema kuwa uchunguzi umebaini kuwa video ya ngono iliyodaiwa kuwa ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Tanzania, Josephat Gwajima ilitengenezwa.

Mei 7 mwaka huu, kuna video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na watu wasiojulikana ikionyesha mtu anayefanana na mchungaji huyo akiwa na mwanamke asiyefahamika  faragha.

Akizungumza na Mwananchi jana Lugola alisema kuwa polisi wanawahoji watu wawili kuhusiana na tukio hilo.

“Uchunguzi bado unaendelea. Video ile ilitengenezwa,”alisema Lugola alipoulizwa na gazeti hili.

Video hiyo inayodaiwa kuwa Gwajima inamuonyesha Gwajima akiwa faragha na mwanamke wakifanya tendo la ngono na mtu anayedaiwa kuwa Gwajima ndiye alikuwa akichukua video hiyo kwa kutumia kamera ya mbele ya kifaa ambacho hakionekani.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kwa kushirikiana  Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI)

walianza uchunguzi wa video hiyo iliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Taarifa yake Jeshi hilo lilitoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza video hiyo kwa maelezo kuwa ni kosa la jinai na kuwataka waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu kwani uchunguzi unaendelea.

Akizungumza na waandishi, Gwajima alisema kanisa hilo litasonga mbele katika utoaji huduma huku akibainisha aliyechimba shimo atatumbukia mwenyewe na mtego alioutega mwenyewe.

Mei 8 mwaka huu Grace, mke wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alizungumzia kuhusu video hiyo inayomuonyesha mtu mwenye sura kama ya mumewe, akisema si yeye kwa kuwa anamfahamu vyema.

Grace alisema anafahamu ukweli wa video hiyo na kamwe haiwezi kumyumbisha kwa maelezo kuwa anamfahamu vyema mumewe.

“Mimi ni kama simba, ukweli naufahamu, namfahamu mume wangu na kumuamini na ukweli huo hakuna mtu anayeweza kuubadilisha.”

“Nipo pamoja na yeye na nitasimama na yeye. Mungu akiwa upande wetu hakuna atakayeweza kuwa juu yetu,” alisema Grace.

Wakati Grace akizungumza mamia ya waumini wa kanisa hilo walionekana wakimshangilia na kuruka ruka kwa furaha.

 


Advertisement