Magaidi wadai Sh3.4 bilioni kuachia madaktari wawili waliowateka Kenya

Thursday May 16 2019

 

Nairobi. Watekaji wanaodhaniwa ni kutoka kundi la kigaidi la Al-Shabaab la nchni Somalia wanaowashikilia madaktari wawili kutoka Cuba waliowateka nchini Kenya na kutaka kulipwa Sh150 milioni za nchi hiyo ili kuwaachia.

Madaktari hao waliotekwa katika eneo la Mandera nchini Kenya karibu na Somalia Aprili 12, 2019 wakitokea nyumbani kwenda kazini.

Madai hayo yametolewa kupitia kwa viongozi wa kimila nchini Kenya waliokwenda katika maeneo ya ndani kati ya miji ya Buale na El-Ade katika Mkoa wa Jubaland nchini Somalia.

Hilo ndilo eneo ambalo madaktari hao, Herera Corea na Landy Rodriguez walionekana mara ya mwisho wakiwa hai mbele ya wazee hao waliotumwa kufanya majadiliano ya kuachiwa kwao.

Baada ya siku kadhaa za majadiliano, wazee hao kutoka Mandera na Bulahawo wamethibitisha kuwa madaktari hao wako hai na wanatoa matibabu kwa wanajamii katika mazingira yanayodhibitibiwa.

“Wanaonekana wanalindwa na wanatoa huduma za tiba kwa wananchi,” alisema ofisa usalama akiwanukuu wazee hao.

Lakini maofisa wa Serikali katika eneo la Mandera wamepinga taarifa hizo wakisema hazijawa rasmi.

Habari zinasema mamlaka nchini Kenya zimetuma wazee hao wa kimila kwenda kufanya majadiliano zaidi kuhusu kiwango hicho.

Taarifa nyingine zinasema madaktari hao kutoka Cuba walitekwa na majambazi waliowakabidhi kwa wanamgambo wa Al Shabaab ambao waliomba kulipwa fedha hizo kutoka wazee wa kimila.

Majambazi hao walitumika kutokana na uhasama kwa kibiashara katika eneo la Mandera baada ya madaktari hao kufanikisha kupunguza gharama za matibabu katika eneo hilo.

Timu ya wanausalama kutoka Cuba walikwenda nchini Kenya na kutembelea eneo la Mandera ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwatafuta madaktari hao waliotekwa nyara. 

Madaktari waliotekwa ni miongoni mwa wengine 100 waliowasili nchini humo Juni 2018. Kutokana na tukio hilo, madaktari wengine waliokuwa wamepangwa katika maeneo ya Wajir, Garissa na Tana waliondolewa na kupangiwa majukumu katika nchi nyingine.

Askari polisi mmoja kati wawili waliokuwa wanawasindikiza madaktari hao aliuawa katika tukio hilo.

Dereva aliyekuwa anawasafirisha kuwapeleka kazini anashikiliwa na polisi na amekuwa akifanyiwa mahojiano.

Advertisement