Yanga wasema Makambo amekwenda Horoya kupima afya, wapokea barua ya Ubelgiji

Thursday May 16 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema straika, Heritier Makambo amekwenda kupima afya katika klabu ya Horoya FC ya Guinea.

 

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi usiku, Mei 16 2019 Dk Msolla amesema bado hawajaongea kuhusu bei, kwani kuna klabu nyingine kutoka Ubelgiji imeleta barua ikimtaka Makambo.

 

Amesema kuwa Makambo bado amebakiza mkataba wa mwaka moja Yanga lakini yupo sokoni na atauzwa Guinea au Ubelgiji kwa kuangalia ofa nzuri.

 

Amesema hayo huku kukiwa na taarifa kuwa straika huyo amesaini kuchezea Horoya kwa mkataba wa miaka mitatu.

 

"Kama amesaini itakuwa ni mkataba wa awali tu, lakini si mkataba rasmi, kwa sababu sisi tuliwaambia akipita vipimo vya afya ndio tungeongea nao ofa yetu," alisema Dk Msolla.

 

Dk Msolla amesema kuwa Makambo ameondoka kwa kibali cha klabu hiyo ya Jangwani akisindikizwa na Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera.

 

"Nimewaambia wachezaji wangu kuwa hapa Yanga ni pazuri, ukionyesha juhudi tu unapata soko. Makambo amejituma na ndio maana sasa anatakiwa na klabu nyingi, ukiacha Horoya kuna klabu ya Ubelgiji imeleta barua, tutaona ni timu gani imeleta kubwa,," alisema kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars.

 

Leo jioni Makambo aliiambia Mwananchi kuwa amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia klabu ya Horoya FC ya Guinea.

Advertisement