Waafrika waliposhindwa kuwaondoa wakoloni kwa vita, hapo kuna funzo

Kwa kiasi kikubwa historia inaonyesha mengi ya makundi ya wapigania uhuru wa Afrika, hayakufanikiwa moja kwa moja katika kuziondoa tawala za kikoloni katika bara hili.

Kuanzia waasi wa Malagasy nchini Madagascar dhidi ya ukoloni wa Ufaransa, Mau Mau ya Kenya dhidi ya Uingereza, African Nationald Congress cha Afrika Kusini (ANC) dhidi ya utawala wa kibaguzi na Front de Libération Nationale (FLN) wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa mwaka 1954 hadi 1962.

Unyama wa kutisha na mauaji ya halaiki yalifanyika wakati wa mapambano katika maeneo mbalimbali. Wapigania uhuru walioshikwa na vikosi vya Wakoloni walikumbana na mateso mabaya kupita kiasi, hadi kufikia hatua ya kuombwa radhi au kulipwa fidia.

Lengo kuu la wapigania uhuru ilikuwa ni kuwaondoa Wakoloni kwa mtutu wa bunduki. Hilo ndio nasema halikuwezekana moja kwa moja. Ila haipingiki kwamba mapambano yao yalikuwa chanzo kikubwa cha Wakoloni kuondoka na kutoa uhuru kwenye sahani.

Hata yale makundi yanayosemwa kwamba yalifanikiwa kutumia nguvu dhidi ya wakoloni na kufanikiwa, bado kuna ukakasi katika maelezo hayo.

Makundi yenyewe ni waasi wa Frelimo wa Msumbiji, PAIGC wa Guinea Bissau na makundi ya waasi wa Angola.

Ukweli ni kwamba, kufanikiwa kwao hakukutokana na nguvu zao moja kwa moja, ila ni baada ya kutokea mapinduzi mwaka 1974 yaliyoangusha utawala wa siasa kali kule Ureno yalitia chachu.

Mapinduzi hayo ndio yakachangia Ukoloni wa Ureno kukosa nguvu barani Afrika na kufukuzwa kwa nguvu katika mataifa waliyotawala.

Hapa ni kusema kwamba, utawala wa Kireno ulianza kupigwa mtama kule shinani, ulipodondoka ndipo hapohapo wazalendo wa Kiafrika wakaitumia nafasi hiyo kuwafurusha.

Pengine bila mapinduzi yaliyotokea Ureno kwenyewe, huenda makundi hayo yangeendelea kusota katika mapambano.

Kushindikana kuwatoa wakoloni kwa nguvu, kulitokana na uwezo wa tawala hizo katika mbinu za kimapambano, silaha, maendeleo ya kiuchumi na uzoefu.

Swali muhimu lilibaki; Je! Waafrika walipaswa kufanya nini baada ya kushindwa kuziondoa kwa nguvu tawala za kikoloni?

Ukombozi wa Afrika lilibaki kuwa jambo la lazima. Swali hilo linajibiwa na Waafrika wenyewe; njia za amani na kwenda katika meza ya mazungumzo, ndio iliyokuwa imebakia.

Hata katika Tanganyika wakati huo, wapo machifu walioendesha vita dhidi ya wakoloni. Ila uhuru ulipatikana kwa amani baada ya waliobaki kuiangalia historia na kuona kwamba adui huyu hatutamweza kwa mtutu wa bunduki.

Ukiidurusu historia ya Afrika, nyakati za uhuru unaona mataifa mengi yalipata uhuru kwa njia ya amani.

Nieleweke vizuri; sina maana kwamba walioingia vitani walikuwa wajinga, ama hawakupaswa kufanya hivyo, la, ilikuwa sahihi kuingia vitani dhidi ya ukoloni.

Ila zaidi nimependezwa na ile sanaa yao ya mapambano, kutoka harakati za vita hadi harakati za amani, baada ya kuelewa nguvu za adui yao.

Sanaa hii ni somo kubwa na la kuzingatia katika ulimwengu wa sasa.

Hivi karibuni maofisa na askari 217 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi JWTZ waliondoka kwenye kulinda amani Darfur nchini Sudan.

Wanajeshi wetu pia wapo Congo na mataifa mengine. Kuna nchi zina migogoro isiyokwisha ndipo Umoja wa Mataifa (UN) au Umoja wa Afrika (AU) hupeleka walinzi wa amani.

Vita na vurugu zinazoendelea ndani ya Afrika zinawahusisha Waafrika wenyewe kwa wenyewe. Wapo ambao wameshindwa kukaa meza moja kuleta amani kwa faida ya mataifa yao.

Ikiwa mababu wa Afrika walikubali kukaa meza moja na mkoloni, adui yao wa muda mrefu, aliyewanyanyasa na kuwaonea, inashindikana vipi Waafrika kwa wenyewe kukaa pamoja na kutatua matatizo yao kwa amani?

Katika Afrika, hasa nchi za maziwa makuu na kati ya Afrika kuna makundi ya muda mrefu yanaendesha vita visivyokwisha.

Anayeumia ni mama, mtoto wa Kiafrika. Hakuna mtu ananufaika na mapambano haya. Inawalazimu waiangalie historia ya mababu zetu ili wajifunze.

Vita visivyotoa ushindi upande wowote hakuna sababu ya kuendelea navyo.

Vita huzidisha dhiki balaa kwa raia. Tafuta mbinu nyingine ya kusukuma mbele madai yako si lazima kwa vita ili pia hawa walinda amani wabaki salama katika mataifa yao.

Historia isibaki tu katika vitabu, tuitumie kwa faida ya kizazi cha sasa. Mabadiliko si lazima yaletwe kwa mtutu wa bunduki.