Mtanzania afungwa miaka 30 kwa kusafirisha heroin Kenya

Wednesday June 12 2019

Hakimu Mkazi Mombasa, Edgar Kagoni,kenya,mtanzania, mwananchi habari

 

Mombasa. Mtanzania aliyetuhumiwa kusafirisha kilo 10.2 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya fedha Za Kenya Sh30 milioni amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Pia, Hussein Masoud Eid pia amepigwa faini ya Sh90 milioni za Kenya. Iwapo atashindwa kulipa fedha hizo atatumikia miaka mitano zaidi jela.

Hakimu Mkazi wa Mombasa, Edgar Kagoni katika hukumu aliyoitoa leo Juni 12, amesema adhabu kali zitasaidia kuzuia mtu asishawishike kujihusisha na biashara ambayo imekuwa na athari mbaya kwa vijana wa Kenya.

“Ilivyokuwa kwamba mtuhumiwa anaonekana hakuwa peke yake kwa sababu alikuwa anapita njia, nitatoa hukumu kali siyo tu kumuadhibu kwa kukubali kutumika na wanaomiliki madawa hayo, lakini pia kuzuia watu wengine wanaoweza kushawishika kusafirisha madawa hayo ya kulevya.

Eid kupitia wakili wake, Jared Magolo, aliomba kupunguziwa adhabu akisema mteja wake ni mgeni na alikuwa mbali na familia yake kwa kipindi kirefu. Hapo awali mwendesha mashtaka wa serikali alitaka mtuhumiwa apewe kifungo cha maisha.

Magolo amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu mtuhumiwa alikuwa amefungwa, na alikuwa amejirekebisha na yuko tayari kuungana na jamii iwapo ataachiwa huru.

Advertisement

Kwa kuwa amejirekebisha, Magolo amesema mteja wake anahitaji kwenda kuungana na jamii kuwasimamia watoto wake wanne.

Wakili aliiomba mahakama kutowaingiza watoto wadogo wa mshtakiwa katika adhabu hiyo kwa kumfunga baba yao ambaye hawajamuona kwa muda wa miaka mitatu.

Hakimu Kagoni hata hivyo alisema alikuwa ametumia uamuzi wake wa kutompa mshtakiwa kifungo cha maisha ingawaje sheria inatoa nafasi ya kifungo hicho kwa kosa hilo.

Eid alifunguliwa mashtaka pamoja na Othmani Hamisi Tinje na Mwenda Hamisi ambao waliachiwa baada ya mahakama kukosa ushahidi wa kutosha unaowahusisha wao na kosa hilo.

Watu hao Masoud, Tinje na Hamisi walikanusha kutenda kosa hilo katika hoteli ya Regency Park mjini Mombasa.

Wakati wakiwakamata watuhumiwa hao, polisi walikamata dola za Marekani 6,100, Sarafu za Madagascar, fedha za Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE.

 


Advertisement