Dar, Mwanza vinara msongamano wa watu mwaka 2018

Muktasari:

Mwaka 2018, Tanzania ilikadiriwa kuwa na watu milioni 54 ambao waliongezeka kutoka milioni 52 waliokuwapo mwaka 2017. Kati ya watu hao, milioni 27.6 sawa na asilimia 51.1 ni wanawake na wanaume walikuwa milioni 26.5 sawa na asilimia 48.9


Dodoma. Dar es Salaam na Mwanza ni kati ya mikoa minne iliyotajwa kuwa na msongamano mkubwa zaidi wa watu mwaka 2018.

Mikoa mingine inayofuatia kwa idadi kubwa ya watu ni Kagera na Kilimanjaro, huku Mkoa wa Lindi ukiwa na idadi ndogo zaidi.

Hayo yameelezwa bungeni leo Alhamisi, Juni 13, 2019  na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango  alipokuwa anawasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa  mwaka 2018 na mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20.

“Dar es Salaam ilikuwa na msongamano mkubwa zaidi wa watu…watu 3,695 kwa kila kilomita moja ya mraba ukifuatiwa na Mwanza (watu 373.1), Kagera (watu 119.6) na Kilimanjaro watu 104,” amesema Dk Mpango.

Mkoa wa Lindi amesema ulikuwa na idadi ndogo zaidi ya watu kwa kilomita moja ya mraba ikiwa na wastani wa watu 14.9, ukifuatiwa na Katavi (watu 16.1) na Ruvuma watu 24.8 kwa kila kilomita moja ya mraba.