Wananchi washangaa pato la kila mmoja kuongezeka kwa Sh100,000 kwa mwaka

Friday June 14 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya Serikali ya Tanzania kusema kipato cha kila Mtanzania kimeongezeka kwa Sh100,000 mwaka 2018, baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti juu ya kauli hiyo iliyotolewa na Waziri wa Fedha na mipango, Dk Philip Mpango.

Mpango ametoa kauli hiyo wakati anasoma taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kwamba wastani wa pato la kila Mtanzania lilifika Sh2.4 milioni mwaka jana kutoka Sh2.3 milioni za mwaka 2017 sawa za ongezeko la Sh100,000 kwa kila mwananchi.

Katika akaunti yake ya Twitter, Mkuyra! (@Gervasmgaya3) ameandika: “Kwa upande wangu kuanzia mwaka 2015 kurudi nyuma nilikuwa na uhakika wa kupata Sh20,000 kwa siku kutokana na kazi yangu lakini kuanzia 2016 hata Sh2,000 ya kurudi nayo nyumbani imekuwa ni janga. Hilo pato nahisi limeongezeka kwa wabunge siyo raia wa Tanzania.”

Mtumiaji mwingine wa mtandao huo, [email protected] (@smailmohmd86) aliandika “Hivi hawa hizi takwimu huwa wanazitoa wapi watu hatupati hata Sh10,000 wao wanasema pato limeongezeka mpaka Sh100,000.”

Kwa upande wake, Hamisi Suluhu (@sululu_succi) alitoa elimu kwa watumiaji wengine wa mtandao huo waliokuwa wanajadili Bajeti inayowasilishwa na Serikali kwa mwaka 2019/20.

Yeye ameandika “Nahisi wanazungumzia GDP per capital income, ambayo huwa inatafutwa kwa kutumia jumla ya thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa ndani ya nchi kwa mwaka kisha wanagawanya na wastani wa idadi ya watu kwa mwaka husika.”

Advertisement

Katika mtandao wa Instagram nako, wananchi wana maoni tofauti. Mmoja wa watumiaji wa mtandao huo anayejitambulisha kama Chriss_mapembe ameandika “Hivi Serikali kwa nini wasiwe wa kweli tu, inakuwaje wanatuongopea huku tukiona kweupe…kwani mkisema hali ngumu inakuwaje, takwimu hizo mnazipata wapi bila kutuuliza sisi?”

Pirlo_Mkongwe, naye mtumiaji wa mtandao huo alikiri ongezeko hilo na namna ya tofauti. Kwenye ukurasa wake, ameandika: “Ni kweli asemacho maana pato langu lilikuwa Sh2,000 lakini hivi sasa ni Sh500, nakula mihogo utasema nguruwe pori.”


Advertisement