Watu 58 wauawa jijini London tangu Januari 2019

Muktasari:

Wakazi wa Jiji la London wameanza kupata hofu kutokana na mfululizo wa matukio ya mauaji baada ya vijana wawili kuuawa jana Ijumaa Juni 14, 2019 na kufikisha idadi ya watu 58 waliouawa tangu Januari, 2019.


London, Uingereza. Vijana wawili wameuawa katika matukio tofauti maeneo ya Wandworth na Greenwitch umbali wa maili 12 kutoka jijini London, Uingereza.

Wakati mmoja wa vijana hao akiuawa kwa kuchomwa kisu, mwingine amepigwa risasi. Matukio hayo yametokea jana Ijumaa Juni 14, 2019.

Mauaji hayo yamefanya matukio ya mauaji jijini London kufikia 58 kuanzia Januari, 2019 huku watatu watatu leo Jumamosi Juni 15, 2019 wakiripotiwa kujeruhiwa kwa kuchomwa visu katika eneo la Clapham.

Polisi wanawashirikia watu 14 wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo.

Taarifa zinaeleza kuwa kijana wa kwanza alichomwa kisu saa 10:42 jioni na kufariki dunia licha ya watoa huduma kujaribu kuokoa maisha yake.

Zinafafanua kuwa kijana mwingine alipigwa risasi eneo la kuegesha magari na kuzua hofu jijini humo huku watu wakikumbuka rekodi ya mauaji ya watu 132 katika Jiji hilo mwaka 2018.

Baadhi ya wananchi wamemkosoa meya wa jiji hilo, Sadiq Khan kwa kushindwa kuzuia mauaji hayo yanayoendelea japo mwenyewe amesema anasikitishwa na matukio hayo.

Khan ametuma salamu za rambirambi kwa familia za vijana hao na amelaani mauaji hayo akitaka wananchi kutoa taarifa polisi ili kusaidia kuwasaka wahusika.