Ndugai ataka Taifa Stars kutengewa fedha, wabunge wahoji mawaziri kutokwenda Misri

Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza bungeni jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa timu ya taifa (Taifa Stars) kwenye fainali za Mataifa Afrika (AFCON) nchini Misri. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wabunge wa Bunge la Tanzania wakiongozwa na Spika Job Ndugai wamehoji mambo matatu kuhusu timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ikiwa ni pamoja na Serikali ya Tanzania kutenga fedha kwa ajili ya timu hiyo.

Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na naibu wake, Juliana Shonza kutoambatana na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Misri, maandalizi duni ya timu hiyo na kutotengewa fedha na Serikali ya Tanzania, ni mambo yaliyotikisa Bunge leo Jumanne Juni 25, 2019.

Wabunge wamehoji mambo hayo matatu baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu na Spika,  Job Ndugai kulazimika kumpa nafasi Dk Mwakyembe kutoa majibu ambayo pia hayakuwaridhisha wawakilishi hao wa wananchi.

Wakati Dk Mwakyembe akisema Ndugai aliyekwenda Misri pamoja na wabunge 50 alimuwakilisha vyema, Spika huyo amesema Dk Mwakyembe na naibu wake kutokwenda Misri hakuleti picha nzuri, kutaka Serikali ya Tanzania katika bajeti yake ya 2020/2021 kutenga fedha kwa ajili ya timu hiyo.

Katika fainali hizo Taifa Stars ipo kundi moja na Senegal, Kenya na Algeria. Tayari imeshacheza mchezo wa kwanza na kufungwa mabao 2-0 na Senegal.

Huku akieleza safari ya wabunge wengine 30 watakaokwenda Misri kesho baada ya wengine 50 kurejea jana, Ndugai aliwataka wananchi wengine kwenda kuishangilia Taifa Stars na kusisitiza kuwa katika kambi ya timu hiyo Misri, kuna mambo hayapo vizuri.

“Tutaongea na waziri mkuu (Kassim Majaliwa) na Waziri wa Michezo katika bajeti zinazokuja ikiwezekana mwakani tutajipanga vizuri zaidi lazima waziri wa fedha atenge fedha kwa ajili ya timu ya Taifa,”

“Lazima tupate kiasi fulani hivi cha fedha kuimarisha michezo kwani inajenga utaifa na kuitangaza nchi kiutalii. Misri wanategemea kuingiza Dola milioni 40 (za Marekani) kupitia fainali hizi,” amesema Ndugai.

 

Wabunge wachachamaa

Baada ya maelezo  hayo ya Ndugai, mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliomba mwongozo na kuhoji  sababu za Dk Mwakyembe na Shonza kutoambatana na timu hiyo na kuungwa mkono na mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliyeomba mwongozo kama huo, kudai jambo hilo linasikitisha.

 

 

Dk Mwakyembe ajibu

Ndugai alimpa nafasi  Dk Mwakyembe kujibu jambo hilo, waziri huyo kubainisha kuwa ilishindikana kutengwa fedha kwa ajili ya Taifa Stars kwa kuwa ilikata tiketi ya kushiriki michuano hiyo muda ukiwa umepita.

“Mwaka jana ningeomba kutenga fedha hizo sijui ningeonekanaje. Si kama hakukuwa na fedha hapana, ya kwenda kukaa (Misri) na posho ya kawaida ilikuwepo lakini huu ni ushindani mkubwa na chochote kinachopatikana kinagawanywa kwa wachezaji wote 23.”

“Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusu kocha (wa timu ya Taifa) napenda kuwe na mjadala mpana baada ya mashindano haya,” amesema Dk Mwakyembe.

Waziri huyo aligusia utaratibu wa timu zinazoshiriki ligi nchini Tanzania kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, kubainisha kuwa unahitaji mjadala, “Ndio maana leo Yanga na Simba zinategemea wachezaji wa nje ndio shida hiyo.”

Kuhusu kutokwenda Misri, Dk Mwakyembe amesema, “Kutokwenda sio kitu muhimu sana, ila Taifa langu liliwakilishwa na Spika. Niwapongeze vijana wa Taifa Stars kwa matokeo yaliyotokea, tumecheza na timu (Senegal) ambayo ni namba moja Afrika (kwa ubora wa viwango vya soka) na ya 22 duniani.”

 

Wabunge walia na Dk Mwakyembe

Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga aliomba mwongozo na kusema, “Kule (Misri) ingekuwa bila jitihada za watu binafsi, hakuna bendera na hakuna chochote cha uhamasishaji hali ni mbaya kuliko mataifa mengine, yeye (Dk Mwakyembe)  alistahili kusherehesha shamrashamra.”

 

Ndugai aweka msimamo

“Nasema kama waziri na naibu wanaendelea kuwa hapa (bungeni) haitoi picha nzuri, kwa yale ya nchi tuyafanye sisi waziri aondoke kwenda AFCON ni jambo kubwa na linagusa watu wengi sana.”

“Wabunge wakienda peke yao na kurudi peke yao haileti picha nzuri. Wajumbe wa kamati ya Bajeti tulimwambia waziri wa fedha kwamba hakuna fedha kwa ajili ya timu ya Taifa wakasema zipo za  timu ya chini ya miaka 17. Waziri wa Michezo mtamnyonga bure hawezi kusema kila siku,” amesema Ndugai.

Ameongeza, “Mwakani au tukishiriki tena AFCON lazima pesa iwepo, timu ya Taifa ni timu ya Serikali. Haiwezekani kitu cha kitaifa harafu Serikali haionekani. Serikali lazima ishike bango maana ni timu yake.”