Bashe atoa ushauri kwa Serikali ya Tanzania

Thursday June 27 2019Mbunge wa Nzega (CCM) Hussein Bashe

Mbunge wa Nzega (CCM) Hussein Bashe 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ameishauri Serikali ya Tanzania kuruhusu wakulima wa pamba kuuza moja kwa moja zao hilo kwa wanunuzi ili kuwapunguzia gharama za usafirishaji.

Bashe alisema hayo jana Jumatano Juni 25 2019, alipokuwa akichangia Muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka wa Fedha 2019.

Alisema hadi hivi sasa hakuna wanunuzi wa pamba katika mikoa ambayo wanalima pamba.

Bashe alisema Serikali ya Tanzania imetoa bei elekezi kwa zao hilo ambayo ni Sh1,200 kwa kilo moja lakini bei ya pamba inategemea soko la dunia.

Alisema utaratibu uliowekwa ni wakulima kupeleka pamba katika Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) na hivyo kumlazimu mnunuzi kugharamia usafiri wa kupeleka katika kiwanda.

Alisema ukichanganya na ushuru na kodi anazotozwa mnunuzi inamfanya kununua kwa zaidi ya Sh1,200 kwa kilo.

Advertisement

Bashe alisema taasisi za fedha zikiangalia mkataba zinaona hatari ambazo mfanyabiashara anazo na hivyo kusita  kutoa mkopo.

Aliishauri Serikali kuruhusu wakulima kupeleka moja kwa moja pamba kwa wanunuzi badala ya kupitia AMCOS ili kupunguza gharama mnunuzi.

Pia, alitaka kufutwa kwa Sh100 ambayo inalipwa kwa Bodi ya Pamba ili wanunuzi waweze kumudu bei ya bidhaa hizo.

Jambo la pili, usafiri wa anga, Bashe alisema Serikali imeamua kuwekeza katika sekta ya usafiri huo kwa kutoa kodi kwenye vilainishi (lubricant) jambo ambalo ni la kupongezwa.

“Ninaomba muondoe kodi ya with holding ya asilimia 10 ambapo mfanyabiashara anaponunua ndege anatakiwa kutoa.”

 “Sekta binafsi  hawanunui ndege kwa fedha taslimu, wananunua kwa mkopo, kwa hiyo down payment anayolipa kwa mujibu wa sheria zetu anatakiwa kulipa asilimia 10 ya with holding tax.”

Alisema kwa kuondoa itasaidia kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga kwa kuwa na uunganisho wa Shirika la Ndege Tanzania na ndege ndogo ndogo.

Jambo la tatu, suala la ngozi, Bashe alisema  taarifa ya kikosi kazi cha wizara ya mifugo na uvuvi imetaja changamoto mbili za sekta ya ngozi nchini ambazo ni kodi ya mauzo ya nje (Export levy).

Alisema matokeo yake viwanda saba vilivyopo nchini vinashindwa kununua  ngozi kutoka kwa wafugaji kwa sababu ngozi haziuziki nje ya nchi.

“Nawaomba Serikali muwaite wenye viwanda musaini nao mikataba ya ufanisi, muwasimamie waweze kusindika ngozi hii na kuongeza thamani,”amesema.

Jambo la nne, Bashe aliipongeza Serikali kwa kutoa msamaha kwa mvinyo unaozalishwa kwa ndizi lakini akashauri kuongeza wigo kwa kuongeza zao la zabibu.

Alisema zabibu ina changamoto ya vifungashio jambo ambalo linamfanya msindikaji kushindwa kushindana na wazalishaji wa nje ya nchi.

Alisema katika mpango wametenga Sh10 bilioni katika ngozi lakini ushauri wake fedha hizo zipelekwe katika kilimo cha zabibu ili wakulima wa zao hilo mkoani  Dodoma waweze kunufaika.

Advertisement