Nyama ya nyumbu yampandisha kortini mtumishi wa hifadhi ya Ikona

Muktasari:

Mfanyakazi wa Jumuiya ya Wanyamapori ya Ikona aliyekamatwa na vipande 231 vya nyama ya nyumbu amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi ya wilaya ya Serengeti.

Serengeti. Mtumishi wa Hifadhi ya Wanyamapori ya Ikona,  amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Serengeti kwa kosa la kukutwa na nyama ya nyumbu.

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Emmanuel Zumba akizungumza mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Ismael Ngaile leo Jumatano Juni 26, 2019, amedai kuwa Thomas Mugabo (56) anakabiliwa na kosa moja la uhujumu uchumi.

Akisoma hati ya  mashitaka katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 60/2019  Ngaile amesema alikamatwa Juni 24, 2019  Saa 2 usiku katika eneo la kituo cha wageni cha jumuiya hiyo kilichoko Robanda, akiwa na nyama ya nyumbu vipande 231 sawa na nyumbu mzima mwenye thamani ya Sh1,430,000.

Hakimu Ngaile amesema kutokana na kosa lake kuangukia kwenye uhujumu uchumi, mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote na amepelekwa mahabusu hadi Julai 10, mwaka huu itakapotajwa tena.