Kiongozi wa mbio za Mwenge amgomea Mkuu wa Wilaya ya Mwanga

Muktasari:

Mwenge wa Uhuru unakimbizwa wilayani Mwanga, miongoni mwa kazi inazofanya ni kuzindua miradi mbalimbali. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na wa maji ambao umebainika kujengwa chini ya kiwango.

Mwanga. Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Mzee Mkongea Ally amemgomea Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson kuzindua  mradi wa maji uliogharimu zaidi ya Sh200 milioni.

Mradi huo upo katika Kijiji cha Kwakoa kwa madai kuwa thamani ya fedha zilizotolewa hazilingani na ujenzi wa mradi huo.

Akikagua ujenzi wa mradi huo jana Jumatano, Juni 26, 2019, kiongozi huyo alimuagiza mkuu huyo wa wilaya  ndani ya wiki mbili awe amewasaka waliohusika  na ubadhirifu wa fedha za mradi.

Amedai kuwa kuna ubadhirifu wa fedha nyingi katika mradi huo.

“Baada ya kufanya ukaguzi wa ujenzi wa mradi huu,  tumetilia shaka taarifa za ujenzi, utaratibu unaelekeza vifaa vyote vya ujenzi  vipimwe kabla ujenzi haujaanza, cha kushangaza  fedha zilizotolewa za mradi huu ni Sh205 milioni na utaratibu wa ununuzi haukutendeka na fedha zimetumika,” amedai Mkongea.

“Kuna ubadhirifu  wa fedha kinyume na utaratibu uliowekwa, thamani ya fedha katika mradi huu haionekani, hivyo sitaweza kuuzindua, tunachokuomba mkuu wa wilaya wahusika wote watafutwe  popote walipo na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesema Mkongea.

Kaimu Mhandishi wa ujenzi  wa Wilaya ya Mwanga, Musa  Njuki amesema wakati ujenzi wa mradi huo unaanza hakuwepo, alihamia Mwanga mwaka 2018.

 “Nilipohamia mwaka 2018,  nilikuta tenki hili la maji limekamilika na mimi kama mhandisi wa maji , ninapoenda mahali lazima nijiridhishe na kile nilichokabidhiwa, lakini nilikuta vipande vya nondo vilivyotumika, nilienda kupima na nilijiridhisha,” alisema Njuki.