Zitto ataka Bunge kuibana Serikali ya Tanzania kuhusu kukopa

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe

Muktasari:

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshauri yafanyike mabadiliko ya kisheria ili Bunge liweze kuipangia Serikali ya Tanzania kiwango cha fedha inachotakiwa kukopa ili kupunguza kuongezeka kwa Deni la Taifa na kuhakikisha mikopo husika inatumika kikamilifu katika miradi ya maendeleo.

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema kuna umuhimu wa Bunge kuipangia Serikali ya Tanzania kiasi cha fedha inachotakiwa kukopa ili kupunguza kuongezeka kwa Deni la Taifa, mikopo husika kutumika kikamilifu katika miradi ya maendeleo.

Alitoa kauli hiyo jana jioni Jumatano Juni 26, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa muswada wa sheria ya fedha mwaka 2019 unaotarajiwa kupitishwa leo Alhamisi Juni 27,2019.

“Mwaka huu tunatarajia kukopa Sh2.3 trilioni kama mikopo ya kibiashara lakini sasa hivi Serikali inahangaika kutafuta mikopo ya miradi mbalimbali ya maendeleo.”

“Waziri wa fedha siku za hivi karibuni alikuwa Marekani na timu yake na walikutana na watu wa Benki ya Standard Chartered kuomba mkopo wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) wa Dola bilioni 1.5 kuanzia Morogoro mpaka Dodoma na kwenda mpaka Isaka,” alisema Zitto.

Alisema mkopo huo unaombwa lakini unakwenda katika ujenzi wa reli inayonufaisha nchi nyingine, si Tanzania.

“Ukitazama ukuaji wa bandari, bandari ya Kigoma inakua kuliko zote, mwaka jana imekuwa kwa asilimia 43.7 na inayofuata ni bandari ya Tanga,  lakini bandari ya Mwanza ambako reli (ya kisasa) ndio inakoelekea kujengwa mwaka jana imekuwa kwa chini ya asilimia moja.”

“Juzi nilishangaa Rais wa Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) alikuja nchini na Serikali ikampeleka kuangalia SGR na wakazungumzia kuifanya Rwanda kuwa kitovu kwa maana ya reli kwenda huko na Congo kuchukua mizigo Rwanda. Hii maana yake tunaiua Tanzania na Bandari ya Kigoma itakuwa haina maana yoyote,” amesema Zitto.

Aliongeza, “Hili naona ni uhujumu kwa nchi yetu,  na njia pekee ya kuzuia hali hii ni kuhakikisha mikopo tunayokopa nje kujenga reli na kuipeleka nchi nyingine, Bunge likatae ili lielekeze mikopo inayokusanywa iende sehemu itakayoleta maendeleo kwa ajili ya nchi yetu.”

Kuhusu kuporomoka kwa bei ya mazao na namna ya kuwalipa wakulima, Zitto alishauri Serikali ilete muswada wa sheria wa kuunda mfuko wa ushuru wa bei ili kuhakikisha zinachangwa fedha na ikitokea bei za soko la dunia inaporomoka, fedha hizo ziweze kuwafidia wakulima nchini.

“Hii itaondoa mgogoro wa bei za mazao za kilimo. Serikali ilifanyie kazi kwa kuanzisha mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa wakulima ambako ndani yake kutakuwa na fao la bei ili kuondoa tatizo hilo,” alisisitiza.