Mlinzi aieleza Mahakama ya Wilaya Ilala Dar es Salaam jinsi alivyokatwa panga

Sunday June 30 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkazi wa Banana Ukonga ambaye ni  Mlinzi shirikishi, Maulid Hamis (35) ameileza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi alivyokatwa kwa panga kichwani na mshtakiwa Nassoro Idrisa  wakati akiwa katika  kazi yake hiyo.

Aliyaeleza hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya jinai namba 342 ya mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Mujaya na Wakili wa Serikali, Aziza Muhina.

Akitoa ushahidi kwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, Maulid  alidai kuwa Machi 3, 2018  majira ya  saa 5 usiku walikuwa katika ulinzi shirikishi pamoja na wenzake maeneo ya Sabasaba kandokando ya  bonde la mto Msimbazi.

“Tukiwa hapo tulipata taarifa kuwa katika maeneo hayo kuna nyumba ambayo haijamalizika inakaliwa na watu wanaojihusisha na matukio ya unyang’anyi na uporaji hivyo tulikwenda na kuizunguka nyumba hiy,” alieleza Hamis mahakamani hapo.

Aliendelea kudai kuwa baada ya kulizunguka wakaingia ndani ili wasitoe mwanya kwa mtu kutoroka na walipoingia walimkuta mshtakiwa Nassoro akiwa amelala ndani ya nyumba hiyo.

“Tulimuamsha, tukajitambulisha kuwa sisi ni walinzi shirikishi na kumuuliza katika nyumba hii, Nassoro wewe upo kama nani, akasema mlinzi na mimi na wenzangu tukamwambia kama kweli ni mlinzi atupe namba ya simu ya mwenye nyumba, akasema hana, hivyo tukaona tuondoke naye hadi polisi Stakishari,”  alieleza shahidi huyo wa upande wa mashtaka.

Advertisement

Alidai kuwa aliposikia neno polisi, alianza kukimbia kwa kuwa mimi sikuwa naye mbali nilianza kumkimbiza na tulipofika umbali mdogo, Nassoro aligeuka na kunifuata kisha akachomoa panga na kunikata kichwani  nikaona giza nikaanguka chini.

“Nikiwa nimeanguka chini Nassoro alinivamia na kunikaba shingoni hata hivyo na mimi nilimng’ang’ania kwa nguvu zangu zote, akaning’ata kidole gumba lakini wenzangu wakawa wamefika wakati huo damu ilikuwa ikiendelea kunitoka,”alieleza Maulid.

Nakuongeza kuwa wenzake waliendelea yeye alipelekwa polisi akapewa PF3 na baadaye akapelekwa katika hospitali ya Amana ambapo alipatiwa  matibabu.

Baada ya shahidi huyo wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake, mshtakiwa Nassoro alimuuliza maswali kama ifuatavyo.

Mshtakiwa Nassoro : Shahidi wewe unaitwa nani?

Shahidi Maulid: Maulid Hamis

Mshtakiwa Nassoro: Una uhakika gani hilo jina ni la kwako?

Shahidi Maulid: ni la kwangu na ndiyo lipo katika kitambulisho changu hiki hapa.

Mshtakiwa Nassoro: unafanya kazi gani?

Shahidi Maulid: Mimi nakufahamu wewe na mwanzoni tulikuwa tukifanya kazi ya ulinzi shirikishi pamoja na ulipoacha nakuona mtaani unalala sehemu ambazo hazina hata mwelekeo.

Baada ya mshtakiwa huyo kumaliza kuuliza maswali hayo, Hakimu Mujaya aliiahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, mwaka huu ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Advertisement