Alichokisema hakimu kesi ya vigogo wa Chadema

Muktasari:

Kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe, kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Julai 24 hadi 26, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania imepanga siku tatu mfululizo, kusikiliza ushahidi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema, akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

 

Uamuzi huo ulitolewa jana Alhamisi Julai 4, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati akiahirisha kesi hiyo, iliyosikilizwa kwa siku nne  mfululizo kuanzia Julai Mosi, 2019.

 

Hakimu Simba alisema, mahakama hiyo itaendelea kusikiliza  ushahidi wa upande wa mashtaka kuanzia Julai 24 hadi 26, 2019 na kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanapeleka mashahidi wa kutosha ili kesi hiyo iweze kuisha  kwa wakati.

 

Tumeanza na kasi nzuri ya kusikiliza ushahidi katika kesi hii, napanga tena siku tatu mfululizo kwa ajili ya kusikiliza kesi hii, hivyo upande wa mashtaka nataka mlete mashahidi wa kutosha mahakamani hapa,  alisema Hakimu Simba.

 

Alisema shahidi wa sita katika kesi hiyo ya jinai namba 112/18,  F 5392 Koplo Charles, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, atamalizia kutoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

 

Shahidi huyo ambaye alitoa ushahidi wake kwa siku mbili mfululizo, ataendelea kutoa ushahidi wake Julai 24, 2019.

 

Katika ushahidi wake, koplo Charles alidai, Februari 16, 2018 alipewa jukumu na bosi wake, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, aitwaye SSP John Malulu, kwenda kuripoti mkutano wa Chadema ambao ulikuwa ni mkutano wa ufungaji wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, jimbo la Kinondoni.

 

"Niliambiwa na SSP Malulu kuwa ikifika saa 10:00 jioni ya Februari 16, 2018 niende nikachukue matukio (kuripoti) mkutano wa Chadema wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni, " alidai

 

"Nilijiandaa kwa kuangalia kamera yangu kama ina chaji ya kutosha na ilipofika saa 9:30 alasiri, RCO alinipa gari la kunipeleka katika mkutano huo uliokuwa unafanyika katika viwanja vya Buibui Mwananyamala, wilaya ya Kinondoni," alidai Koplo Charles.

 

Tayari mashahidi watano wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao na miongoni mwa mashahidi hao ni  Daktari  Juma Khalfani (54) kutoka Hospitali Kuu ya Jeshi la  Polisi, Kilwa Road.

 

Katika ushahidi wake Dk Khalfani, alieleza askari waliojeruhiwa katika maandamano ya Chadema, walipigwa na kitu chenye ncha kali na butu.

 

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Salim Msemo, Dk Khalfani alidai askari hao ambao ni PC Fikiri Mtega na Koplo Rahim Msangi, walifikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu baada ya kujeruhiwa katika maandamano yanayodaiwa kuwa ni ya wafuasi wa Chadema, eneo la Mwananyamala, Wilaya ya Kinondoni.

 

Dk Khalfani ambaye pia ni Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi hilo, alidai Februari 16, 2018, majira ya saa 5:40 usiku, akiwa katika wodi ya wazazi, alipewa taarifa na nesi kutoka chumba cha wagonjwa wa dharura kuwa kuna wagonjwa wawili wamefikishwa katika hospitali hiyo huku hali zao zikiwa sio nzuri.

 

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko;  Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.