Vyama vya siasa Tanzania vyawalilia wanahabari wa Azam

Muktasari:

Kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea kati ya Mkoa wa Tabora na Singida na kusababisha vifo vya watu saba wakiwemo watano wa Kampuni ya Azam Media Ltd, baadhi ya vyama vya siasa vimetoa salamu za rambirambi kwa msiba huo.

Dar es Salaam. Baadhi ya vya siasa vimetoa salamu za rambirambi kufuatia vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media Limited vilivyotokana na ajali ya barabarani.

Ajali hiyo ilitokea leo asubuhi Jumatatu Julai 8, 2019 katika eneo la Kizonzo kati ya Wilaya ya Igunga (Tabora) na Shelui (Singida) ambapo gari aina ya Coaster lililowabeba wafanyakazi wa Azam Media Ltd lililokuwa likielekea wilayani Chato mkoani Geita limegongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa likielekea Dar es Salaam.

Wafanyakazi hao walikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea kwenye sherehe za uzinduzi wa hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato kwa ajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya sherehe hizo zinazofanyika kesho Jumanne.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando amewataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Salim Mhando, Florence Ndibalema, Said Haji, Sylvanus Kasongo na Charles Wandwi huku wa watatu wakijeruhiwa

Ajali hiyo imeua pia madereva wawili wa basi hilo dogo na lori.

Kufuatia ajali hiyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimetoa salamu za rambirambi na pole kwa vyombo vya habari kwa kampuni hiyo kwa kupotelewa na wafanyakazi watano.

“Chadema inatoa pole kwa tasnia ya habari nchini, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo. Wakati tunawaombea marehemu wapate pumziko la amani, tunawaombea pia majeruhi uponaji wa haraka warejee katika siha njema,” imesema taarifa ya Chadema.

Mbali na Chadema, Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kushtushwa na vifo hivyo. “Pole kwa Azam, pole kwa familia za marehemu,” amesema Katibu mwenezi wa chama hicho, Ado Shaibu.

Ajali hiyo pia imeigusa CCM ambapo katika taatifa yake iliyotolewa katika mtandao wa Twitter imeeleza masikitiko yake.

“Uongozi wa Chama cha Mapinduzi umepokea kwa mshtuko taarifa za ajali iliyogharimu watu saba wakiwemo wanahabari wa kituo cha Azam. Tunatoa pole kwa wafiwa kwa familia ya Azam Media,” imesema taarifa ya CCM.