Ukosefu wa fedha, chanzo cha upungufu wa nguvu za kiume

Muktasari:

Uhitaji busta ya kusisimua nguvu za kiume kama una fedha

Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa ukikosa fedha unaweza kutumia kila aina ya dawa kusisimua misuli ya uume ili kuupa nguvu za awali, lakini usipate matokeo unayoyatarajia.

Tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume na kupanda kwa gharama za maisha vinakwenda sambasamba.

Hivi karibuni ulifanyika utafiti katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam uliobaini kuwa asilimia 24 ya wanaume wana tatizo la nguvu za kiume.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk Pedro Pallangyo akizungumza na Mwananchi Mei 18 alibainisha kuwa utafiti huo uliofanyika mwaka 2016, uliwachunguza wanaume 18,441 wote wakazi wa Kinondoni, wenye umri wa miaka 47.

Asilimia 24, karibu robo waliripoti kuwa na shida katika nguvu za kiume.

Machi mwaka jana, Serikali ilitangaza rasmi kuzitambua aina tano za dawa za asili baada ya kuzikagua. Hizo ni Ujana, IH Moon, Coloidal Silver, Sudhi na Vatari.

Pamoja na tafiti hizo kuhusisha baadhi ya magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu, saratani kuwa yanasababisha upungufu wa nguvu za kiume, utafiti uliofanywa mwishoni mwa mwaka jana na Northwestern Mutual ya Marekani umebaini kuwa fedha pia ni chanzo cha wanandoa na wapenzi kupungukiwa nguvu za kiume na kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa.

Utafiti huo umebaini kuwa mbali ya fedha kuongeza idadi ya wanaume wasiomudu vyema kujamiiana kwa wenza au wake zao, pia ni chanzo cha msongo wa mawazo.

Watu wanne kati ya 10 walioshiriki kwenye utafiti huo walikiri kuwa fedha zinaathiri uwezo wao wa kuwaridhisha wenza wao kwenye tendo la ndoa.

Mmoja kati ya watano walisema kuwa wamekuwa wakiingia kwenye migogoro ya kimapenzi na wenza wao walau mara moja kwa mwezi.

“Msongo wa mawazo utokanao na ukosefu wa fedha, unashusha hamu ya kufanya mapenzi.

“Kwa sababu nguvu nyingi hutumika kuwaza, kupanga, kuhofia ukosefu wa fedha, ikiwamo kufanya kazi kwa muda mrefu na kujikuta wakiishia kuchoka bila kupata wanachotaka au kupata kiasi kisichokidhi mahitaji ya familia na kuathiri mfumo mzima wa kumudu tendo la ndoa, ” alisema Azra Alic wakati wa kuwasilisha utafiti huo uliofanyika katika nchi tano ikiwamo Marekani ukihusisha miji yake mikubwa.

Ushuhuda

Kuhusu hilo, Ally Amiri (43) alisema kwa siku alikuwa anaweza kujamiiana hata mara tatu na akamaliza mara mbili kwa kila mzunguko, lakini sasa mara moja anaitafuta.

“Nilikuwa ninafanya kazi benki moja iliyokuwa ya Serikali kabla ya kubinafsishwa na nikawa miongoni mwa waliopunguzwa kazi.

“Hapo ndiyo mtihani ulipoanza nikiwa nina miaka 40 nilistuka mke wangu akinilazimisha kujamiiana, ilhali alikuwa anakataa akilalamika kuchoka kutokana na shughuli yangu,” alisema.

Alisema kuna wakati hali inakuwa ngumu hadi hakumbuki mara ya mwisho alitamani au kulifanya lini.

“Asikuambie mtu, mapenzi bila fedha hayanogi kwa wanawake na wanaume, itakuwa na nguvu gani ilhali kiakili sipo sawa, sijala vizuri na sina uhakika wa kula watoto hawajakwenda shule, nadaiwa kodi.

“Kwa misingi hiyo tatizo la kukosa nguvu za kiume litahamia na Temeke ‘kiume’ kwa sababu hali ya maisha ni ngumu, ” alisema.

Mwita Maurya anasema, “huwezi kupiga vitatu, vinne na mtu ambaye hujui baada ya hapo utampa nini.

“Huna nauli, hana nauli, hajala hata soda hujamnunulia halafu ujifanye fundi, kwa hali hii zitapungua sana nguvu, ” anasema.

Anasema akifikiria madeni aliyonayo anaona tendo hilo ndilo linamuongezea mzigo, hivyo kujikuta anapunguza siku za kulifanya na sasa ana miaka 39 kijana kabisa lakini hana spidi aliyokuwa nayo miaka tisa au 10 iliyopita.

Akitoa ushuhuda kuhusu hali hiyo Moureen Jose (sio jina lake halisi) anasema kuwa mpenzi wake akiwa na fedha anafurahia zaidi tendo hilo kuliko akiwa hana.

“Kwanza huwa ninamlazimisha kwa kumhurumia ninajua akiwa hana fedha hapendi kujamiiana.

“Sijui inakuwaje, akiwa na fedha ninajua kabla sijaziona kwa sababu ya mbwembwe zake anakuwa kama kijana wa miaka 20 hachoki na muda mwingi anazungumzia suala hilo,” anasema Moureen.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa ya Wagonjwa wa Akili Mirembe, Dk Damas Andrea anasema ni kweli kuna uhusiano kayi ya msongo wa mawazo na uwezo wa kujamiiana.

Anasema kama akili haipo sawa, sio rahisi mwili kufanya kazi hiyo sawasawa.

Anasema miongoni mwa vitu vinavyotajwa kuathiri utendaji tendo la ndoa ni pamoja na kutopata muda wa kupumzika ikiwamo usingizi.

“Ukiwa na msongo wa mawazo moja kwa moja huwezi kulala vya kutosha, hivyo utakuwa umepata athari ya moja kwa moja ya kutokuwa na nguvu ya kushiriki tendo hilo,” anasema Dk Andrea.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Nkungu Daniel pia anasema kuwa msongo wa mawazo ni chanzo cha upungufu wa nguvu za kiume na ukosefu wa hamu ya kufanya tendo la ndoa.

Dk Nkungu anasema mwili usipokuwa katika hali yake ya kawaida ikiwamo kujaa msongo wa mawazo unaotokana na mshtuko kama wa msiba, hauwezi kufanya kazi kama kawaida ikiwamo kujamiiana.

“Tofauti hapo ni chanzo cha msongo wa mawazo kinatofautiana, lakini kwa namna yoyote iwayo ukiwa nao lazima utendaji tendo la kujamiiana utaathirika, kwa sababu huanzia kwenye ubongo na ukiwa na msongo ubongo unaathirika moja kwa moja,” anasema Dk Nkungu.

Anasema mtu ambaye anapata fedha za wastani akizikosa kabisa anaweza asiwe na msongo, lakini ambaye alizoea kuwa nazo nyingi zikiisha anaweza kuupata.

Anafafanua kuwa pia kuna tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine namna anavyokabiliana na msongo wa mawazo na aina zake.

Anasema si lazima kinachompa mawazo mtu fulani kitampa na mwingine.

Mtaalamu wa saikolojia na viungo, Lauren Dummit ambaye pia ni mwanzilishi wa Triune Therapy Group ya Los Angeles alisema baadhi ya wanaume wanapokuwa hawana fedha hukosa kujiamini na kushindwa kujadili masuala kuhusu mapenzi, “hiyo hupoteza hamu ya kujamiiana kwa sababu licha ya mwanamke kuwa na hamu, mwanamume ndiyo anaweza kuamua tendo hilo lifanyike au laa.”

Alisema zipo tafiti za kisayansi mbali na hiyo waliyofanya zikielezea ukaribu kati ya msongo wa mawazo unaotokana na ukosefu wa fedha na upungufu wa nguvu za kiume.

“Msongo wa mawazo unapunguza nguvu za kiume, hususan unapohusisha mwanamume kushindwa kutimiza majukumu ya kifamilia” alisema Dk Kate na Lauren walioshiriki kwenye utafiti huo.