Breaking News

Bosi mpya TIB awatoa hofu wateja wa benki hiyo

Monday July 15 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kaimu mkurugenzi mkuu wa benki ya (TIB) Corporate, Fred Luvanda amesema hajui kwa kina sababu za kuondolewa kwa mtangulizi wake lakini amewahakikishia wateja wa benki hiyo wataendelea kupata huduma kama kawaida kwakuwa mabadiliko ya uongozi wa juu yaliyofanyika hayaathiri shughuli za benki za kila siku.

Luvanda ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 15 mwaka 2019 wakati wa mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya benki hiyo.

"TIB Corporate haiko chini ya usimamizi ya Benki Kuu (BoT) ni mabadiliko tu ya uongozi wa juu yaliyofanyika, aliyeondolea ni mkurugenzi mtendaji lakini huduma nyingine zinaendelea kama kawaida ingekuwa chini ya usimamizi wa BoT menejimenti na bodi vingevunjwa lakini hapa nimeletwa tu mimi kusaidia kuifikisha benki hii mahali ambapo Serikali inataka," amesema Luvanda.

Amesema wateja wa benki hiyo ya biashara hawapaswi kuwa na taharuki kwa mabadiliko hayo yaliyotokea kwani BoT hufanya mabadiliko kama hayo inapoona kuna haja ya kulinda amana za watu.

Kuhusu sababu halisi za kuondolewa kwa mtangulizi wake (Frank Nyabundege) amesema leo ndiyo siku yake kwanza kufika kazini hapo bado hajafahamu kwa kina mwenendo halisi ya benki hiyo, anafahamu vyema baada ya kukaa na menejimenti.

Alipoulizwa kuhusu mikakati ya kuinusuru benki hiyo na hali ya mwenendo uliotajwa na BoT amesema ni mapema kueleza kwakuwa yeye ni mgeni ofisi hapo lakini kuna mikakati ya benki hiyo ambayo bado ipo ndani ya wakati, aliitaka menejimenti na wafanyakazi wote kufanya kazi kwa bidii.

Advertisement

Aidha juzi Jumamosi 13, 2019 BoT ilitangaza kusitisha ukurugenzi wa Frank Nyabundege baada ya kuongoza benki hiyo kwa miaka mitano tangu mwaka 2014, sababu za mabadiliko hayo zilielezwa kuwa ni mwenendo usioridhisha.

BoT ilitumia mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa sheria ya sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2016 na kusema hatua hiyo inalenga kuboresha usimamizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali.

Hata hivyo mwenendo wa benki hiyo yenye wateja zaidi ya 3800 kwa mwaka uliopita na robo ya kwanza ya mwaka huu haukuwa mbaya kwani repoti ya Desemba mwaka 2018 ilitengeneza faida ya Sh1.3 bilioni kabla ya makato ya kodi na robo ya kwanza ya mwaka huu faida ni Sh935 milioni.

Vilevile mpaka Machi 31 mwaka 2019 mtaji wa benki hiyo ulikuwa ni Sh40.2 bilioni huku kiwango cha mikopo chechefu kikiwa ni asilimia 5.1.

Advertisement