Bendi ya polisi yageuka kivutio, Kangi ajitosa kusakata muziki

Monday July 15 2019

 

By Rehema Matowo,Mwananchi [email protected]

Geita. Bendi ya polisi nchini Tanzania imegeuka kivutio kwa viongozi na wananchi waliofika kwa ajili ya hafla ya ufunguzi wa nyumba 20 za polisi zilizofunguliwa leo Jumatatu Julai 15, 2019 eneo la magogo mjini Geita.

Uzinduzi huo umefanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli ambapo bendi hiyo ilionyesha uhodari wake wa upigaji mzuri wa tarumbeta uliombatana na mbwembwe za wapigaji ulikuwa kivutio kilichowafanya viongozi washindwe kuvumilia kukaa kwenye viti na kushuka kutoka jukwaa kuu na kwenda kuwatunza

Bendi ya polisi ambayo makao yake makuu ni chuo cha polisi Moshi mkoani Kilimanjaro iliyokuwa na wakata mauno machachari iliwaacha watu hoi huku waziri wa mambo ya ndani akishindwa kujizuia na kuungana nao kukata mauno.

Wakata mauno hao wamekuwa kivutio pia kwa Rais Magufuli  namna wanavyokata viuno na kupongeza jeshi hilo kwa kutoa burudani nzuri na kusema jeshi la polisi limeiva kisawasawa katika mambo yote.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alishindwa kujizuia na kuamua kwenda kusakata muziki na kuonyesha naye ni mjuzi wa kucheza hali iliyoibua shangwe kutoka kwa watu waliohudhuria shughuli hiyo.

Advertisement