Bongo movie, Swahilflix kumleta Will Smith Tanzania

Muktasari:

 Msani kutoka nchini Marekani, Will Smith anatarajiwa kuwa mmoja wa wageni watakaohudhuria uzinduzi wa kuonyesha filamu za Tanzania kupitia mtandao wa Swahiliflix. 

Dar es Salaam. Wasanii wa filamu nchini Tanzania kwa kushirikiana na mtandao wa kuonyesha filamu za Kiswahili ‘Swahiliflix' wanatarajia kumleta Tanzania msanii maarufu wa Marekani, Will Smith.

Kiongozi wa wasanii hao, Steve Nyerere, ameyasema hayo jana Jumatatu Julai 15,2019 alipokuwa akitambulisha mtandao huo kwa waandishi wa habari.

Steve alisema uzinduzi wa uonyeshwaji wa filamu hizo unatarajiwa kufanyika Julai 31, 2019 ambapo pamoja na waalikwa wengine, msanii Willy Smith ambaye mbali ya kuwa msanii wa filamu anatarajiwa kuwa mmoja wa wageni kutoka nje.

Alisema  wasanii hao ni wadau muhimu kwao ukizingatia ni watu waliopiga hatua katika tasnia ya filamu muda mrefu.

"Pia siku hiyo ya uzinduzi tutaangalia filamu za wasanii wa hapa nchini ikiwemo ya JB na Ray ambao wao tayari wana filamu mpya," alisema Steve.

Baadhi ya wasanii hawakusita kueleza furaha yao kwa ujio wa mtandao huo akiwemo Aunt Ezekiel alisema anaiona tasnia ya filamu kuzaliwa upya na kuahidi kwamba hawatawaangusha mashabiki wao kwani watajitahidi kutengeneza kazi bora.

Naye mchekeshaji Themed Mariaga maarufu 'Mkwere' alisema kwa muda mrefu watu waliopo nje ya Tanzania wamekuwa wakihitaji kuona vichekesho vyao lakini hawakuwa na namna kwa hivyo kupitia mtandao huo watawafikia kirahisi.

Awali, Ofisa Masoko wa Swahiliflix Tanzania, Nazir alisema kupitia mtandao huo watu wataweza kupakua filamu na kuangalia muda wowote watakao kupitia simu zao za mkononi na kwenye kompyuta.

Jacob Steven alisema soko la filamu halikufa bali nilikuwa likipitia katika kipindi cha mpito na kwa kuwa teknolojia imekuwa sasa nao wanatakiwa kubadilika kwani wengi wa mashabiki wao kwa sasa wanashinda kwenye simu zao hivyo na filamu zinatakiwa ziwafikie huko.