Rais Magufuli asisitiza bei elekezi zao la pamba ni Sh1,200

Rais Magufuli

Muktasari:

Wakati bei elekezi ya Sh1, 200 kwa kilo ilipotangazwa Mei 2, 2019, bei ya pamba katika soko la dunia ilikuwa senti 77 ya Dola ya Kimarekani kwa kilo; kiwango ambacho kimeshuka kufikia kati ya senti 65-67 ya dola ya Kimarekani.

Mwanza. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amesisitiza msimamo wa Serikali kuwa bei elekezi ya kununua zao la pamba ni Sh1, 200 kwa kilo.

Rais Magufuli amesema anayetaka kutoa bei tofauti la zao hilo alipe bei ya juu zaidi lakini siyo chini ya bei elekezi iliyotangazwa na Serikali Mei 2, 2019 wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu iliofanyika kijiji cha Kasekese wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

“Hakuna kununua pamba chini ya Sh1, 200 kwa kilo. Labda walipe zaidi ya hiyo,” amesema Rais Magufuli alipohutubia wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma za tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza leo Julai 15, 2019

 

Msimamo huo wa Rais Magufuli umekuja muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwahakikishia wakulima wa pamba kuwa Serikali kupitia Benki Kuu (BoT) kukubaliana kudhamini mikopo ya wanunuzi wa pamba kwenye benki na taasisi za fedha ili kumaliza hofu ya hasara iliyotokana na bei ya zao hilo kushuka katika soko la dunia.

Akizungumza na wakazi wa Ana jana Jumatatu Julai 15, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ufumbuzi huo umepatikana baada ya kikao chake na wanunuzi wa pamba, wakuu wa mikoa inayolima pamba, wawakilishi wa mabenki na BoT kilichofanyika juzi Jumapili.

“Hofu ya wanunuzi ilikuwa ni hasara na kushindwa kurejesha mikopo benki na taasisi zingine za fedha; tatizo hilo sasa limeisha baada ya Serikali kupitia BoT kukubali kutoa dhamana ya mikopo hiyo,” alisema Waziri Mkuu alipohutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mbutu wilaya ya Igunga mkoani Tabora

Wakati wa uzinduzi wa msimu, bei ya zao hilo kwenye soko la dunia ilikuwa senti 77 ya dola ya Kimarekani lakini ikashuka hadi kati ya senti 65 hadi 67 ya dola.

Kwa mujibu wa Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba, Bozi Ogola, anguko hilo liliwapa wanunuzi hofu ya kupata hasara iwapo wangelipa bei elekezi ya Sh1,200 bila kupata dhamana ya Serikali kwenye benki na taasisi za fedha wanakochukua mikopo.

Kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia inadaiwa ni matokeo ya mgogoro wa kibiashara kati ya China ambao ndiyo wanunuzi wakuu wa pamba na wamiliki wa viwanda vingi vya nguo duniani na Marekani ambao ndiyo wanunuzi wakuu wa nguo kutoka viwanda vya China.

Akizungumzia soko la pamba na mazao yake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), Marco Mtunga ameiambia Mwananchi kuwa kila Mmarekani mmoja anavaa nguo zinazotokana na kilo 21 za pamba kila mwaka kulinganisha na kiwango cha kilo tatu kwenye nchi zinazoendelea, zikiwemo za Kiafrika.

 

Hofu ya hasara miongoni mwa wanunuzi ilisababisha shehena ya pamba iliyokusanywa kutoka kwa wakulima kukusanywa katika maghala ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) kwa zaidi ya miezi miwili bila wakulima kulipwa.

Kutokana na kukosa malipo, baadhi ya wakulima katika maeneo ya Sapiwi na Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu, walifikia uamuzi wa kuzuia pamba yao iliyokusanywa katika maghala ya vyama vyao vya ushiriki kuchukuliwa na wanunuzi hadi watakapolipwa fedha zao.

“Hatutaruhusu gari yoyote kusomba pamba kutoka Amcos hadi tulipwe. Hatuko tayari kukumbwa na yaliyotokea kwa wenzetu (wakulima) wa korosho kule mikoa ya Kusini,” Peter Maduhu, mmoja wa wakulima kijiji cha Sapiwi wakati wa tukio la kuzuia malori ya wanunuzi kusomba pamba