NEC kuanza uboreshaji wa Daftari, Kihamia atoa mwongozo

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, Athuman Kihamia

Muktasari:

Tume ya Uchaguzi(NEC) imewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura utakaozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Moshi Julai 18,2019.

Arusha. Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, Athuman Kihamia amewataka wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, kutumia siku saba za uboreshwaji wa Daftari la Wapiga kura kwa njia ya Kieletroniki (BVR), kujiandikisha na wasitarajie muda zaidi kuongezwa.

Akizungumza jijini hapa jana Jumatatu, Julai 15, 2015 alipofika kujionea mafunzo yanayotolewa kwa waandikishaji wasaidizi jijini Arusha,  alisema NEC imejipanga kikamilifu kuhakikisha shughuli nzima ya uboreshaji daftari inakwenda vizuri kwa sababu wamejipanga  kuondoa kasoro zilizokuwepo kipindi cha nyuma.

“Tunataka maandalizi na shughuli nzima ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura iende vizuri, kwa baraka za Mwenyezi Mungu kama hakutakua na jambo lolote ambalo lipo nje uwezo wa kibinadamu, tutahakikisha uchaguzi unakua huru na haki na malalamiko yaliyokuwepo huko nyuma yamepungua kwa asilimia 90,” alisema Kihamia.

Alisema uboreshaji wa Daftari la Wapiga kura utaanza Julai 18, mwaka huu katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, baadaye watahamia katika mikoa mingine kuendelea na utaratibu huo ambao alisema unafanyika mara mbili katika misimu ya uchaguzi .

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua uboreshaji huo katika Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro na uandikishaji unawalenga wale ambao hawajawahi kujiandikisha na ambao kadi zao zimepotea, kufuta waliofariki dunia na  kuhuisha taarifa zao.

Wakati huohuo, Kihamia alisema kabla ya kufika Arusha, alitembelea Jimbo la Singida Mashariki kunakotarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo na wagombea wa vyama vya siasa 12 wameshachukua fomu na mwisho wa kurejesha fomu hizo ni Julai 18,2019.