TCU yavifungulia vyuo vilivyofungiwa kudahili

Mkurugenzi wa Uratibu na Udahili wa tume hiyo, Dk Kokuberwa Katunzi-Mollel

Muktasari:

  • Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imesema baadhi ya vyuo vikuu vilivyofungiwa usajili mwaka jana vianze kudahili wanafunzi.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imesema baadhi ya vyuo vikuu vilivyofungiwa udahili mwaka jana, vimeruhusiwa kufanya hivyo mwaka huu.

Akizungumza wakati wa Maonyesho ya TCU yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jana Jumatatu Julai 15, 2019, Mkurugenzi wa Uratibu na Udahili wa tume hiyo, Dk Kokuberwa Katunzi-Mollel amesema vyuo hivyo vimeruhusiwa kufanya udahili baada ya kukidhi vigezo vilivyotakiwa.

Huku akiahidi majina ya vyuo vingine vilivyoondolewa kwenye  kifungo hicho kutajwa baadaye,  alivitaja baadhi ya vilivyo funguliwa kuwa ni Chuo kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU),  Chuo kikuu kishiriki cha Marian cha Bagamoyo, Chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala (KIU) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo (AMUKTA).

Tayari dirisha hilo la udahili limefunguliwa kwa awamu ya kwanza kuanzia jana Jumatatu Julai 15 hadi Agosti 10, 2019.

Amewataka wanafunzi wanaotaka kujiunga na elimu ya juu kuanza udahili na kazi ya TCU ni kusimamia utaratibu.

“Dirisha limeshafunguliwa na safari hii wanafunzi wanaweza kuomba kupitia mitandao kwenye simu zao za mkononi au kompyuta, sio lazima wasafiri kwenda nyumbani,” alisema.

Amesema maonyesho hayo yanawasaidia wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kuchagua vyuo wanavyotaka kujiunga kwa sababu, vyote huwa vinaonyesha kozi zinazotolewa kwenye vyuo vyao katika maonyesho hayo.