Mayweather hana mpango wowote kurudiana na Pacquiao

Muktasari:

Mabondia hao wawili walipambana mwaka 2015 katika pambano lililotangazwa sana na kuingiza fedha nyingi na kuisha kwa Mayweather kushinda kwa pointi.


Floyd Mayweather hana mpango wowote wa kurudi katika masumbwi na kupambana tena na Manny Pacquiao baada ya wawili hao kuvaana katika pambano lililoingiza fedha nyingi mwaka 2015, rafiki yake mkubwa, Leonard Ellerbe alisema jana Jumatano.

Ellerbe, ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Mayweather Promotions, aliiambia tovuti ya boxingscene.com kuwa si kurudiana na Pacquiao tu, hata pambano litakalomuingizia fedha nyingi hazitamshawishi kurejea ulingoni.

Inaaminika kuwa Mayweather alipata dola 300 milioni za Kimarekani katika pambano hilo aliloshinda kwa pointi na kutengeneza fedha nyingine zaidi ya dola 600 milioni kutoka katika vyanzo vingine.

Kocha wa muda mrefu wa Pacquiao, Freddie Roach alisema wiki iliyopita kuwa angependa bondia huyo Mfilipino angerudiana na Mayweather baada ya kipigo kilichomchanganya katika pambano la kwanza.

Hata hivyo, Mayweather atakuwa pembeni ya ulingo akiwa upande wa Pacquiao katika pambano la ubingwa wa dunia dhidi ya Keith Thurman jijini Las Vegas Jumamosi, na Ellerbe anasema hakuna uwezekano wa pambano la marudiano kufanyika.

"Floyd hana nia kabisa," Ellerbe aliiambia boxingscene. "Hana nia yoyote. Amekuwa akifanya hayo (kupigana ngumi) katika maisha yake yote. Na baada ya muda, mtu huwa unachoka. Ameachana na mchezo huu."

Ellerbe alisema kwa sasa Mayweather anafurahia maisha ya kustaafu ndondi.