Mahabusu, wafungwa kesi za 'kuku' kuachiwa huru

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga

Muktasari:

Miongoni mwa watakaonufaika na amri hiyo ya Rais Magufuli ni pamoja na wafungwa na mahabusu wa kesi ndogondogo zikiwemo za wizi ya shati, simu za tochi, udokozi na kuokota kuni ndani ya maeneo ya hifadhi.

Mwanza. Mahabusu wenye kesi ndogondogo na wafungwa ambao watabainika kubambikiwa kesi, watoto, wazee na makundi mengine yenye mahitaji maalum wanatarajiwa kufutiwa kesi na vifungo vyao baada ya Rais John Magufuli wa Tanzania kuagiza uhakiki wa kuwabaini kufanyika kwenye magereza yote nchini.

Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma jana Rais Magufuli alisema uhakiki huo unaongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga.

“Nimeagiza (Wizara ya Katiba na Sheria, ofisi ya DPP na vyombo vingine vinavyohusika na Mahakama) waendelee kupitia kila gereza kufanya uhakiki kwa watu wanaoshikiliwa kimakosa waachiwe; leo (jana Alhamisi) maofisa hao watakuwa kwenye gereza la Kasungamile na Geita,” alisema Rais Magufuli katika hotuba yake

 “Siwezi kutawala nchi yenye machozi na watu wanaosikitika kwa unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa,” aliongeza Mkuu huyo wa nchi.

Miongoni mwa watakaonufaika na amri hiyo ya Rais Magufuli ni pamoja na wafungwa na mahabusu wa kesi kama za wizi wa shati, simu za tochi, udokozi na kuokota kuni ndani ya maeneo ya hifadhi.

Amri hiyo inatekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria, ofisi ya DPP na mamlaka zingine za dola zinazohusiana na uendeshaji wa mashauri mahakamani, likiwamo jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye jukumu la kukamata na kupeleleza.

 

DPP aanza utekelezaji

Utekelezaji wa amri hiyo tayari umeanza baada ya juzi DPP kuutangazia umma kupitia kwa waandishi wa habari jijini Mwanza uamuzi wa kuwafutia vifungo na mashtaka wafungwa na mahabusu 325 kutoka katika magereza saba ya mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga.

Magereza ambayo mahabusu na wafungwa wake wamenufaika na uamuzi huo wa DPP na idadi ya waliofutiwa vifungo na kesi kwenye mabano ni Mugumu (52), Butimba (75), Bariadi (100), Bunda (24), Kahama (43), Musoma (6) na Shinyanga walikoachiwa watu 25.

Askari Polisi wanane waliokuwa wakikabiliwa kesi namba 1/2019 ya kusafirisha kilo 319 za dhahabu na rushwa ya Sh305 milioni katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mwanza ni miongoni mwa wafungwa na mahabusu 75 walionufaika na uamuzi huo wa Serikali kwa  mashtaka dhidi yao kufutwa na kuachiwa huru jana.