Usiyoyajua kuhusu January Makamba

Dar es Salaam. Wengi wanamfahamu zaidi January Makamba aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na mbunge wa Bumbuli katika ulingo wa siasa, lakini kuna mengi ambayo baadhi ya watu hawayajui kuhusu mwanasiasa huyo tangu akiwa na umri mdogo hadi sasa.

Wapo wengi tu ambao nao hatua waliyoifikia au kazi wanayoifanya pengine haikuwa katika ndoto zao, mambo yalibadilika njiani na kuwalazimu kuendana nayo.

Hali hii hujitokeza kwa watu mbalimbali, wako wengi tu wanaofanya kazi katika kile ambacho hakikuwa katika ndoto zao za awali, wala hawakuwahi kuwaza lakini kutokana na sababu za hapa na pale au mtu fulani kumvutia kwa anachokifanya na yeye hujikuta ameingia huko.

Ni hivyo hivyo kwa January Makamba, ndoto yake haikuwa kuwa mwanasiasa bali alikuwa na ndoto tofauti alivyokuwa mdogo, lakini zote ziliyeyukia njiani kadri alivyokuwa akikua, akisoma na kazi alizokuwa akizifanya kwa nyakati tofauti.

Katika mahojiano yake na Mwananchi yaliyofanyika akiwa bado waziri, Makamba anasema mtu akiwa mdogo anakuwa na ndoto mbalimbali.

“Ukiwa na umri wa miaka minne unataka kuwa polisi, na miaka sita unataka kuwa muuguzi baada ya kuona mtu amevaa nguo rangi nyeupe au baadaye unataka kuwa mwanajeshi. Baadaye ukiona wachezaji wanashangiliwa unataka kuwa mwanamichezo.

Anasema kuanzia nyakati za umri mdogo hadi kiwango cha elimu ya sekondari mambo yalikuwa yakibadilika sana na wakati anasoma kidato cha nne alikuwa akipenda fani ya sayansi akichukua mchepuo wa masomo kemia, baiolojia na kilimo. (CBA)

Aliingia kidato cha tano na sita, alichukua masomo ya Historia, Jiografia na Uchumi (HGE), kabla hajajiunga na masomo ya chuo kikuu alibahatika kufanya kazi kwenye kambi za wakimbizi kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu ya juu.

“Kwa sababu kazi ilikuwa nzuri na niliipenda ilibidi niongeze muda hadi nafasi ya chuo ikaondoka. Nikasema kuanza kazi yangu itakuwa ni kutoa huduma ya misaada kwa wakimbizi na kujihusisha na utatuzi wa migogoro inayosabababisha wakimbizi kukimbia maeneo yao.

“Ndio maana niliamua kusoma kozi ya diplomasia ya utatuzi wa migogoro, shahada yangu ya kwanza na ya pili. Nisingekuwa mwanasiasa ningekuwa mwanadiplomasia na mtatuzi wa migogoro,” anasema Makamba.

Hata hivyo Makamba anasema kwamba hajutii kuingia kwenye siasa kwa kuwa ni kazi nzuri inayompa mtu nafasi ya kuhudumia wananchi hasa kuanzia nafasi ya ubunge na uwaziri inayompa heshima kubwa ya kutunga sera, kuanzisha na kushughulikia masuala mbalimbali.

“Huwezi kujutia hii kazi hata siku moja kwa sababu inakupa uzoefu na itakufanya uache alama, historia kama mbunge na waziri. Kitu ambacho kigumu ni mchakato mzima kwenye siasa, ukifeli ni shida na ukifanikiwa sana pia ni shida.

“Shida ya siasa unatengeneza maadui ambao hauwajui, wala sababu zao kuwa maadui kwako huzijui. Kwa hiyo hiki kitu ni kigumu kwa mtu ambaye si mwanasiasa hakupenda kuingia kwenye siasa kama mimi lakini hivi sasa unazoea,” anasema Makamba.

Anafafanua kuwa baada ya kushinda ubunge na kwenda bungeni mwaka 2010, hakuwa mgeni na jengo hilo kwa kuwa alishalizoea akiwa msaidizi wa rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na alishiriki kuandika hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo mwaka 2006.

Kuhusu jina la baba yake

Makamba anasema jina la baba yake aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM linamsaidia lakini kuna muda linamkwaza, kwa sababu Yusuf alikuwa na marafiki wengi na sifa na udhaifu.

“Ukijitokeza kwa marafiki zake (baba) wanalinganisha sifa zake na wewe. Lakini baba alikuwa na udhaifu wake pia nazo wanakulinganisha na wale maadui zake una warithi haraka sana,” anasema Makamba.

Amtaja Kikwete

Anasema Kikwete, ndiye aliyemvutia kwenye siasa kwa sababu alimpa nafasi ya kufanya kazi pamoja kwenye ulingo huo. Awali alianza kufanya kazi na Kikwete alipokuwa akifanya mafunzo kwa vitendo Wizara ya Mambo ya Nje wakati huo Kikwete akiwa waziri katika wizara hiyo kabla ya baadaye kujitosa kugombea ubunge jimbo la Bumbuli mara ya kwanza mwaka 2010.