Balozi Kenya ahoji mahindi ya Tanzania kukwama kuingia nchini humo

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu

Dar es Salaam. Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu amesema ni aibu kwa magari yaliyopakia mahindi kutoka Tanzania kuzuiwa  mpakani wakati raia wa Kenya wanakabiliwa na njaa.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 25, 2019 jijini Dar es Salaam alipokutana na naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe pamoja na viongozi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo  kujadili mpango wa Kenya kununua chakula Tanzania.

Amesema Tanzania na Kenya ni ndugu ni vyema zikaondoa vikwazo vya biashara ili wafanyabiashara kutoka katika nchi hizo waweze kufanya biashara na kusaidiana bila kukwamishwa na taratibu za kiofisi.

“Hamna haja mtu aje anunue mahindi hapa, aende mpaka pale Sirali, Holili au Namanga halafu magari yabaki hapo wiki nzima. Ni aibu watu wana njaa kule Kwale, wana njaa kule Kajiado, magari yanakwama hapo sijui kwa siku ngapi.”

“Unasikia sijui wanasubiri mmoja atie sahihi ndiyo magari yapite, hii siyo sawa. Hatusemi mambo yafanyike kiholela, lakini mambo yafanyike katika ofisi moja ambayo gari ikitoa hakuna haja ya kukaa wiki moja, siku kumi, watu wanabaki wanaumia hapo Taveta,” amesema Kazungu.

Bashe amezitaka taasisi zote zinazohusika kwenye mchakato huo kukaa pamoja na kujadili namna gani wataondoa vikwazo katika mchakato huo ili kurahisisha usafirishaji wa chaula kwenda Kenya.

“Taasisi za serikali zianze kufikiria kibiashara, kaeni muone namna gani mtaondoa ukiritimba, na itakuwa vizuri taasisi zote zinazohusika zikaratibu suala hili kwenye ofisi moja ili kurahisisha biashara,” amesema Bashe.