Waziri asema kigogo wizara ya fedha alikuwa kiunganishi kati ya Serikali, umoja wa Ulaya

Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa amesema aliyekuwa ofisa mwandamizi Wizara ya Fedha na Mipango, Leopold Lwajabe alikuwa kiunganishi kati ya Serikali na Umoja wa Ulaya (EU).

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa amesema aliyekuwa ofisa mwandamizi Wizara ya Fedha na Mipango, Leopold Lwajabe alikuwa kiunganishi kati ya Serikali na Umoja wa Ulaya (EU).

Lwajabe aliyekuwa mkurugenzi wa miradi inayotekelezwa na EU kupitia wizara hiyo, mwili wake ulikutwa wilayani Mkuranga mkoani Pwani Julai 26, 2019 ukining’inia juu ya mti wa mwembe kwa mujibu wa familia yake.

Bashungwa ambaye ni mbunge wa Karagwe ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019 katika misa za mazishi ya ofisa huyo iliyofanyika Kanisa Katoliki Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam.

"Injinia Lwajabe ni kaka yangu, ndugu yangu, rafiki yangu na mtumishi mwenzangu. Mara ya mwisho nilikutana naye Julai 13, 2019  tulisafiri pamoja kwenye ndege tukielekea Bukoba. Nilivyopata taarifa za kifo chake sikuamini kabisa.

"Katika kazi zangu za utumishi kwa wananchi wa Karagwe, Lwajabe amenisaidia sana, nilikuwa namtegemea kuwa kiungo kati ya Serikali na Umoja wa Ulaya, nitamkumbuka kwa mengi kwa upendo wake,  alipambana vya kutosha tukapata fedha zikajenga barabara ya kiwango cha lami," amesema Bashungwa.