Nchi wanachama wa SADC zasuasua kutekeleza mkakati wa viwanda

Muktasari:

Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeelezwa kutoridhishwa na namba nchi za jumuiya hiyo zinazotekelezwa mkakati wa viwanda unaomalizika awamu ya kwanza mwaka 2020.

Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mkakati wa viwanda kwa nchi za Jumuiya hiyo utakaomalizika katika awamu ya kwanza mwaka 2020.

Dk Stergomena amesema licha ya mafanikio kadhaa kuonekana katika baadhi ya maeneo ndani ya mkakati huo, endapo nchi hizo zinahitaji kufanikiwa katika mkakati huo, zinalazimika kujiuliza ni kwa nini maeneo mengine utekelezaji wake unasuasua  na hatua gani zifanyike.

Kwa mujibu wa SADC, mkakati huo wenye lengo la kuongeza kasi ya kuimarisha ushirikiano na ushindani  wa kiuchumi kutoka katika nchi zisizokuwa wanachama wa SADC, unatekelezwa katika vipindi vya miaka mitano kuanzia 2015-2063 na awamu ya kwanza itafikia ukomo mwakani. Mkakati huo unahusisha maeneo matatu ya Viwanda, Ushindaji na Mtangamano wa Kikanda.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne Agosti 13, 2019 wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri, 16 wa Nchi za SADC, uliokwenda sambamba na tukio la Waziri wa Mambo ya Nje Profesa Palamagamba Kabudi kukabidhiwa kijiti cha kuongoza baraza hilo kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu wa Namibia na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

“Kati ya maeneo 50 ya yaliyopo katika utekelezaji wa awamu ya kwanza, ni maeneo matano tu yaliyokamilika, maeneo 46 bado yako katika utekelezaji na saba bado hayajaingia katika utekezaji, hali hii inaashiria wazi kwamba juhudi bado zinahitajika zaidi katika ngazi ya Taifa na ukanda,“ amesema Dk Stergomena.

“Kama tunahitaji kufanikiwa hatua hizi, tunatakiwa kuangalia maeneo hayo kwa nini bado hayajatekelezwa na kitu gani kinatakiwa kufanyika vinginevyo tutakuwa tunaimba wimbo wa viwanda tu lakini maendeleo yatakuwa katika kiwango cha chini.”

Dk Stergomena amegusia pia utekelezaji wa  Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Miundombinu katika mtangamano (RIDMP), utakaofikia ukomo wake 2027. Mpango huo una lengo la kuimarisha sekta usafirishaji, nishati, Teknolojia ya habari na Mawasiliano(Tehama), vyanzo vya maji na hali ya hewa.