Tundu Lissu aitwa Mahakama ya Tanzania

Tuesday August 13 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa hati ya wito wa kufika mahakamani kwa mbunge wa zamani Singida Mashariki, Tundu Lissu kwa ajili ya shauri la maombi yake kuanza kutajwa.

Wito huo kwa Lissu umetolewa leo Jumanne, Agosti 13, 2019 na kusainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Lssu amefungua maombi mahakamani hapo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, kupinga kuvuliwa ubunge wake.

Shauri hilo ambalo litasikilizwa na Jaji Sirillius Matupa limepangwa kutajwa keshokutwa Alhamisi, Agosti 15, 2019.

Katika hati hiyo ya wito wa kufika mahakamani, Mahakama hiyo imemtaka kufika mahakamani tarehe hiyo bila kukosa na pia awasilishe vielelezo vyote ambavyo anakusudia kuvitumia, katika kesi hiyo.

Advertisement

Mwanasheria huyo Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amekuwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kunusurika katika jaribio hilo la mauaji kwa takribani miaka miwili, tangu  Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa.

Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai Juni 28, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge huku akitaja sababu mbili.

Spika Ndugai alizitaja sababu hizo ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ikiwa ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Lissu alifungua shauri la maombi  Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa hati ya shauri hilo la maombi namba 18 la mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo, impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Pia, anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge.

Vilevile  Lissu anaomba Mahakama hiyo impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Advertisement