35,000 wajeruhiwa, 8,000 wafariki kwa ajali za bodaboda

Muktasari:

  • Takwimu zilizotolewa mapema wiki hii na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani zimeonyesha kuwa watu 35,231 walijeruhiwa kutokana na ajali za bodaboda huku vifo vikifikia 8,004 kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi 2018.

Dar es Salaam. Jeshi la polisi kikosi cha Usalama Barabarani limetoa takwimu kuhusu hali ya ajali nchini kwa miaka 10, zilizoonyesha watu 35,231 wamejeruhiwa kufuatia ajali za pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’.

Takwimu hizo pia zimeonyesha kuwa vifo vilivyotokana na ajali hizo kufikia 8,004 kutoka kipindi cha mwaka 2009 hadi 2018.

Akitoa takwimu hizo, Kamanda wa Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani nchini (SACP) Fortunatus Muslimu amesema ajali za pikipiki zimekuwa zikisababisha majeruhi wengi nchini na vifo.

“Jumla ya ajali kwa kipindi cha miaka 10 zilizosababishwa na pikipiki zilifikia 37,421 ambazo zilisababisha majeruhi 35,231 na vifo 8,004,” amesema Kamanda Muslimu.

Akitoa tathmini kwa ujumla, ametaja kupungua kwa ajali za barabarani akitolea mfano kutoka 22,739 za mwaka 2009 mpaka kufikia ajali 3,746 za mwaka 2018.

Akifafanuza zaidi kuhusu ajali za mwaka 2009, alisema zilizosababishwa na madereva zilikuwa 11,059, ubovu wa vyombo vya moto 2,233, mwendo kasi 1,025, makosa mengineyo 2,894, ulevi 221, uzembe wa waendesha pikipiki 2,347, uzembe wa waendesha baiskeli 1,701 na uzembe wa watembea kwa miguu 1,259 na kufanya jumla yake kuwa 22,739.