ABDUL RIDHIWANI PANGAMAWE Miaka 38 ndani ya Msondo Ngoma

Muktasari:

Mwaka 1980 akiwa amefikia nyumbani kwa wajomba zake maeneo ya Mwananyamala, Dar es Salaam akitokea Iringa, Abdul Ridhiwani akiwa na umri wa miaka 16, zikasikika habari za kuondoka kwa mpiga kinanda wa Juwata Jazz, Waziri Ally katika bendi hiyo.

Safari yake ya jijini Dar es Salaam ilikuwa ni kwa ajili ya kuendelea na elimu ya juu katika Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim baada ya kumaliza darasa la saba mkoani Iringa, lakini ghafla akajikuta akiangukia katika muziki. Ilikuwaje?

Mwaka 1980 akiwa amefikia nyumbani kwa wajomba zake maeneo ya Mwananyamala, Dar es Salaam akitokea Iringa, Abdul Ridhiwani akiwa na umri wa miaka 16, zikasikika habari za kuondoka kwa mpiga kinanda wa Juwata Jazz, Waziri Ally katika bendi hiyo.

Ridhiwani akawaambia wajomba zake anamudu nafasi hiyo. Ulitokea ubishani mkali kati yake na wajomba zake kina Ahmad Mlilima.

Wajomba wa Ridhiwani walikuwa mashabiki wa Juwata Jazz na walikuwa wakifahamiana kwa karibu na mwanamuziki Juwata Jazz, Joseph Lusungu ambaye naye alikuwa akiishi Mwananyamala.

“Wajomba zangu wakaniuliza kama nitakuwa tayari kupelekwa katika bendi hiyo nami nikawaambia hakuna wasiwasi wanipeleke tu na nitaitendea haki nafasi hiyo,” anasema Ridhiwani.

Mwanamuziki huyo anasema wajomba zake hawakufanya ajizi wakamchukua hadi nyumbani kwa Lusungu na kumwambia dogo anataka kuziba pengo la Waziri.

Lusungu alimwangalia Ridhiwani, hakuamini kama ameiva kuziba pengo lile. Pengo la Waziri lilikuwa kubwa kuliko umri wa kijana huyo aliyekuwa amesimama mbele yake na kuaminishwa kuwa anaweza kuliziba.

“Anataka kujifunza au? Maana siye pale hatufundishi na wamekuja watu wengi wameshindwa, huyo ataweza kweli?” Ridhiwani anayakumbuka maneno ya Lusungu. Mwishowe kwa shingo upande, Lusungu ambaye kwa sasa ni marehemu alikubali Ridhwani apelekwe katika Ukumbi wa Amana, Ilala kwenye mazoezi ya bendi hiyo.

AFELI MAJARIBIO

Siku ya siku ilifika, wajomba wakamchukua Ridhiwani hadi Amana na kumkabidhi kwa Lusungu aliyemchukua na kumpeleka kwa mwanamuziki mwingine wa bendi hiyo, marehemu Kassim Mponda kwa ajili ya kumfanyia usaili. Kwa mujibu wa Ridhiwani, kinanda kilikuwa kimefungiwa sehemu nyingine tofauti na pale wanamuziki walipokuwa wakifanya mazoezi.

Kwa hiyo sehemu hiyo ilikuwa ni yeye na Mponda tu na akatakiwa kuonyesha ujuzi wake. Hata hivyo, chini ya Mponda, Ridhiwani hakuweza kuonyesha maajabu yaliyokuwa yakisubiriwa, alifeli kufanya kile ambacho Waziri alikuwa akikifanya katika bendi hiyo.

Mponda alimuacha Ridhiwani kwenye kinanda na kupeleka ujumbe kwa Lusungu aliyekuwa ukumbini akiendelea kufanya mazoezi na wanamuziki wengine kuwa yule kijana (Ridhiwani) hakuweza kumudu.

MAAJABU YATOKEA

Wakati Mponda akiondoka, huku nyuma Ridhiwani akawa anaendelea kukichezea kinanda kwa kujifurahisha bila ya uangalizi wa mwanamuziki yeyote.

“Nilikuwa naendelea kukifanya. Nikawa najiuliza nimekosea wapi?”

Wakati Ridhiwani akiendelea kujiuliza, kiongozi wa bendi hiyo, Said Mabera ‘Dokta’ alikuwa akiingia ndani ya ukumbi huo akitokea Mnazi Mmoja kwenye makao Makao Makuu ya Jumuiya ya Wafanyakazi (Juwata).

Akiwa katika mlango wa kuingia ndani ya ukumbi akamuona kijana mdogo akipapasa kinanda kwa kufuata nyayo za Waziri Ally aliyeikacha bendi hiyo na kujiunga na The Revolution (sasa The Kilimanjaro, Wana Njenje).

Mabera hakuamini alichokiona na kukisikia kutoka kwa bwana mdogo yule, bila ya kumwambia kitu akaenda moja kwa moja hadi kwenye ukumbi na kuwaambia wanamuziki wenzake kuwa yule bwana mdogo ni hatari anamudu kuzifuata nyayo za Waziri.

Mponda na Lusungu wakawa watu wa kwanza kumbishia kwa kumwambia kuwa huyo kijana alishindwa usaili.

Baada ya kumsikia Mabera, wanamuziki hao wakakubaliana kwenda kumsikiliza mmoja mmoja bila ya kumshtua kama wanamfuatilia. “Ndipo wakati nikiendelea kupiga kinanda nikawaona wale wazee wakija mmoja mmoja kunisikiliza huku wakijifanya kutokuwa na habari na mimi.

“Sikuacha kupiga nilipiga kopi zote za Waziri Ally na kuwafanya wanikubali, wote waliridhika na uwezo wangu na kuanzia hapo habari ya kujiunga na kidato cha kwanza, Kinondoni Muslim ikaishia hapo,” anasema Ridhiwani na kuongeza wanamuziki wa Juwata Jazz waliamini kuwa awali alikumbwa na mchecheto.

Tangu Oktoba 1980, Abdul Ridhiwani Pangamawe amekuwa mwanamuziki wa bendi hiyo na kuachana na masuala ya shule. Na ndiye mwanamuziki wa pili kukaa muda mrefu katika bendi hiyo bila ya kutoka baada ya Mabera.

Kutokana na umahiri wake wa kupapasa kinanda wanamuziki wa bendi hiyo wakampachika jina la Totoo. Na wimbo wake wa kwanza kupiga kinanda kikakubalika ni Julekha uliotungwa na marehemu Shaban Dede.