ACT- Wazalendo waanza kutamba Z’bar, wasema urais 2020 ni wao

Muktasari:

  • Kwa mara ya kwanza aliyekua Mkurugenzi wa habari Chama cha Wananchi (CUF) Salim Abdalla Bimani amesema chama cha ACT-Wazalendo kitashinda nafasi ya urais visiwani Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao 2020.

Unguja. Kwa mara ya kwanza aliyekua Mkurugenzi wa habari Chama cha Wananchi (CUF) Salim Abdalla Bimani amesema chama cha ACT-Wazalendo kitashinda nafasi ya urais visiwani Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao 2020.

Bimani ameyasema hayo jana Jumanne Machi 19, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika shughuli ya upandishaji wa bendera ya ACT-Wazalendo katika Makao Makuu ya CUF Vuga mjini Unguja.

Amesema hana wasiwasi kwa mwamko walionao Wazanzibar wengi ana hakika chama hicho kitaibuka na kuwa tishio kama ilivyokuwa  CUF hapo awali na hatimaye kupata mafanikio makubwa katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Amesema kwa sasa unaweza kuona wamechelewa kufanya uamuzi hayo lakini ana hakika ari na kasi ya Wazanzibar walio wengi muda mchache ACT-Wazalendo kitakuwa na nguvu isioweza kufananishwa na chama chengine chochote kwa upande wa Unguja na Pemba.

Hata hivyo, amewatoa wasiwasi wale wote ambao bado hawajaamua kufanya uamuzi na kuwataka wajiunge upande wa aliyekuwa katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amehamia ACT-Wazalendo.

Sambamba na hayo amebainisha inaweza isionekane kwa haraka lakini anaamini hata baadhi ya wanachama wa CCM wataipigia kura ACT wazalendo katika uchaguzi mkuu wa 2020 kutokana na kusheheni watu wenye busara na upeo wa kuona mbali.