ATCL kuanza safari za Dodoma kila siku

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi amesema kutokana na ongezeko la abiria, shirika hilo limeanzisha safari za kila siku kwenda Dodoma,  kuanzia Januari 16, 2019

 


Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi amesema kutokana na ongezeko la abiria, shirika hilo limeanzisha safari za kila siku kwenda Dodoma,  kuanzia Januari 16, 2019.

Amesema hivi sasa ndege za shirika hilo zinafanya safari nne kwa siku kwenda Dodoma.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 11, 2019 katika hafla ya kupokea ndege ya pili aina ya Airbus 220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Amesema licha ya kuongeza safari hizo pia wanaendelea kufanya tathmini ya uhitaji ili kuhakikisha Dodoma inaunganishwa na miji mingine ili kurahisisha usafiri wake.

“Kuwasili kwa ndege ni soko la kimkakati kusini mwa Afrika hususani nchi za Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini lakini pia inaongeza uhakika wa kutoa huduma katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu ikiwemo Mwanza, Kilimanjaro na Mbeya,” amesema Matindi.

“Hii ni fursa muhimu katika kuhakikisha biashara yetu inakuwa endelevu na tayari tumefanikiwa kuingia makubaliano usafirishaji wa nyama ya mbuzi inayouzwa nje ya nchi kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa na mashirika mengine.”

Amesema wanaendelea kushirikiana na shirika la ndege la Ethiopia na Misri ili kuendeleza marubani na mpaka sasa wamefikia 50 kutoka 13 waliokuwepo awali na hadi kufikia Aprili, 2019 watakuwa wamefikia 60 huku wahandisi wakiwa 68 kutoka 15.

Amesema wahudumu wa ndege wamefikia 142 kutoka chini ya 20 walioanza nao na mpaka sasa wafanyakazi wa ATCL wanakaribia 300.