ATCL kwenda Zambia, Zimbabwe

Muktasari:

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limetangaza gharama ya nauli kwa safari zake kati ya Dar es Salaam, Harare Zimbabwe na Lusaka Zambia zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

 


Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limetangaza gharama ya nauli kwa safari zake kati ya Dar es Salaam, Harare Zimbabwe na Lusaka Zambia zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa mujibu wa tangazo la shirika hilo lililotolewa leo Januari 16, 2019, nauli ya kwenda Lusaka (Umbali wa kilometa 1,936 kutoka Dar) itakuwa Dola za kimarekani 218 sawa na Sh502,000 kwa safari moja na Dola 374 sawa na Sh862,000 kwa safari ya kwenda na kurudi.

Safari ya kwenda jiji la Harare ambalo lipo umbali wa kilometa zaidi ya 2,200 nauli yake ni Dola za Kimarekani 214 sawa na Sh493,000 kwa safari moja na Dola 317 sawa na Sh726,000 kwa safari ya kwenda na kurudi.

Aidha ATCL ambayo hivi sasa pia ina safari za kimataifa katika nchi tatu (Comoro, Burundi na Uganda) ina jumla ya ndege sita zinzofanya kazi, itakuwa ikifanya safari kati ya miji hiyo kwa siku za Jumanne, Ijumaa na Jumapili.

Ndege hizo za ATCL ni tatu aina ya Bombardier Q400-8, mbili aina ya Airbus A220-300 na moja aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner).

Hata hivyo ndege zake mbili aina ya Bombardier Q400-8 zinatarajiwa kufanyiwa marekebisho madogo (C Check) hivi karibuni ambayo yatachukua hadi siku 21.

‘C Check’ kwa ndege hizo hufanyika pale ndege inapofikisha masaa 4,000 ambayo imeruka angani.