Abiria afia ndani ya basi stendi ya Ubungo

Dar es Salaam. Mwanaidi Said (83), abiria aliyekuwa anasafiri kutoka kuelekea mkoani Tabora, amefariki dunia leo alfajiri akiwa ndani ya  basi kabla ya kuanza kwa safari katika kituo cha mabasi cha Ubungo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Mussa Taibu ameliambia Mwananchi leo Jumapili, Juni 23, 2019 kuwa abiria huyo amekutwa na mauti akiwa ameketi kwenye kiti cha basi hilo linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Kigoma kupitia mkoani Tabora.
“Alikuwa akisumbuliwa na saratani na alikuwa anakwenda mkoani Tabora baada ya kumaliza matibabu yake hapa Dar es Salaam na vyeti vimeonyesha hivyo,” amesema Kamanda Taibu.
Faida Paul ambaye ni mtoto wa Mwanaidi aliyeambatana naye katika safari hiyo, amezungumza na Mwananchi na kusema kuwa mama yake alikuwa mgonjwa na alikuja Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
“Leo tulikuwa tumeanze safari kurudi Tabora na tulikuwa tukisubiri muda tu wa kuondoka. Wakati tunasubiri, ndiyo yakatokea ya kutokea kwa mama kufariki,” amesema Faida.
Kwa mujibu wa Faida, msiba upo Kigamboni na maziko yanafanyika leo.