Abuni mashine ya kuchanganya kemikali za kuzalisha sabuni za maji

Kijana Richard Majaliwa kutoka taaisis ya Don Bosco akionyesha mashine ya kuchanganyia kemikali za kutengeneza sabuni za maji na shampoo.

Muktasari:

  • Mashine ya kuchanganya kemikali za kutengeneza sabuni ya maji na shampoo imebuniwa na kijana kutoka taasisi ya Don Bosco lengo ni kurahisisha utengenezaji wa bidhaa hiyo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.

Dar es Salaam. Mwanafunzi kutoka taasisi ya Don Bosco nchini Tanzania amebuni mashine rahisi ya kuchanganya kemikali za kutengeneza sabuni za maji na shampoo, baada ya kuona kina mama wakitumia muda mwingi na nguvu wakati wa kutengeneza bidhaa hiyo.
Wajasiriamali wengi hasa kina mama huchanganya kemikali za sabuni kwenye beseni au ndoo kwa kutumia mwiko, wakati mwingine wanashindwa kuchanganya vyema.
Akiongea na Gazeti hili jana kwenye Maonyesho ya 43 ya Biashara Kimataifa Sabasaba mwanafunzi Richard Majaliwa alisema, yeye amesomea ufundi umeme wazo la kutengeneza mashine hiyo limekuja baada ya kuona changamoto ambazo mwalimu wa somo la kutengeneza sabuni alizokuwa akikutana nazo.
"Nilikaa tu nikaanza kuchora namna ya kutengeneza hii mashine baada ya kuona kina mama wakikoroga sabuni kwa kutumia mwiko kwenye beseni au ndoo na wakati mwingine wanalazimika kupunguza kiwango kutokana na uchovu," alisema
Mashine hiyo inatumia umeme mdogo ambao mjasiriamali mdogo anaweza kutumia, ina uwezo wa kukoroga lita 200 kwa saa moja na kuchanganya kemikali zote vizuri.
Aidha alisema, kwa njia ya kawaida ndoo ya lita 20 kumaliza kuchanganya hutumia kati ya saa tatu hadi nne kumaliza na mwili unakuwa umechoka.
"Hii mashine inasaidia pia kujiepusha na harufu ya kemikali kwani ukisha weka kwenye tanki unasubiri ilikuwa tayari unaweka vifaa vya kukingia kwenye bomba ambayo umeunganishwa tayari kwa hatua ya pili," alisema
Majaliwa aliongeza kuwa kukamilisha  mashine moja anatumia mwezi mmoja tu, kwa hiyo ni fursa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kuchangamkia fursa hiyo kwani malighafi za kutengeneza zinapatikana nchini
Kwa upande wake Abia Lugisha alisema, "Sisi tuna kikundi cha vikoba moja ya bidhaa tunazotengeneza ni sabuni za maji na huwa tunatumia mikono kuchanganya kemikali ambayo wakati mwingine ina madhara kiafya,"
Alisema mashine kama hii ni nzuri kwa inarahisisha kazi hivyo atakwenda kuzungumza na wenzake kuona namna ya kufanya.