Acacia walimwa faini Sh5.6 bilioni

Muktasari:

  • Mbali na faini hiyo, Acacia pia wamepewa wiki tatu kurekebisha kasoro katika bwawa la kuhifadhi maji taka yenye sumu

Serikali imeipiga faini ya Sh5.6 bilioni Mgodi wa Dhahabu wa Acacia North Mara kwa kwa kutiririsha maji yenye kemikali kwenye makazi, vijito na mito.

Pamoja na faini, mgodi huo pia umepewa muda wa wiki tatu kurekebisha kasoro zilizobainika katika bwawa la kuhifadhi maji taka yenye sumu ambayo uchunguzi wa kitaalam umethibitisha yanavuja na kuingia kwenye makazi ya watu na kuathiri maisha ya binadamu na mazingira.

Uamuzi huo ulitangazwa mjini Tarime jana na Mkurugenzi wa Baraza la Mazingira, Dk Samuel Gwamaka mbele ya mawaziri January Makamba, Ofisi ya Makamu wa Rais  (Muungano na Mazingira) na Dotto Biteko wa Madini waliotembelea na kukagua mfumo wa kudhibiti na kuhifadhi maji taka ya mgodi huo.

"Pamoja na faini, mgodi pia utatakiwa kurekebisha kasoro zilizobainika na kujenga bwawa mbadala ili kudhibiti maji taka yenye kemikali," alisema Dk Gwamaka.

Wakizungumza kwa kupokezana, Makamba na Biteko walisema si nia ya Serikali kuwaadhibu, kuwapiga faini au kufungia shughuli za wawekezaji, lakini inabidi kuchukua hatua hizo kulinda sheria, usalama, maisha ya wananchi na mazingira.

"Tunapenda mrabaha. Tunapenda mapato yatokanayo na dhahabu; lakini tunapenda zaidi usalama na maisha ya wananchi na mazingira yetu," alisema Makamba.

Alionya kuwa Serikali itasitisha kwa muda leseni ya kuendesha mabwawa ya maji taka ya mgodi huo iwapo kasoro zilizobainika hazitarekebishwa kwa muda uliotolewa.

"Hatuufungi mgodi kwa sababu shughuli za uchimbaji hazina tatizo. Tutasitisha leseni ya kuendesha mabwawa na ikibidi tutaufuta kabisa," alisema na kuonya Makamba.

Kwa upande wake, Biteko aliwapongeza wataalam kutoka Nemc, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wizara mbalimbali waliochunguza mfumo wa uhifadhi na udhibiti wa maji taka wa mgodi huo kwa kufanya kazi kwa uzalendo na kuiwezesha Serikali kuchukua hatua.