Acacia yaruhusiwa kusafirisha dhahabu

Muktasari:

Ni kutoka Mgodi wa North Mara uliozuiwa tangu Julai 12, 2019.

Dar es Salaam. Baada ya kuzuiwa kusafirisha dhahabu kwa takriban mwezi mmoja, Tume ya Madini Tanzania imeiruhusu kampuni ya Acacia kuendelea na utaratibu huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Acacia iliyotolewa Ijumaa iliyopita, ilipokea barua ya ruhusa hiyo kutoka Tume ya Madini baada ya ukaguzi uliofanywa na mamlaka hiyo mara kadhaa Julai kujiridhisha kuhusu uzingatiaji sheria na kanuni za madini.

“Acacia imepokea barua ya kuendelea kusafirisha madini kutoka Mgodi wa North Mara baada ya kutimiza masharti. Tume inaamini kuna baadhi ya vifungu vya kanuni za madini za mwaka 2010 vilikiukwa na imeuagiza mgodi kuandaa ripoti ili ithibitishwe mpaka Agosti 16,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Julai 12, Tume ya Madini ilizuia usafirishaji dhahabu kutoka North Mara kwa maelezo ya kutaka kufanya ukaguzi eneo la mgodi huo. Baada ya uchunguzi huo, Julai 17 tume hiyo ilizuia matumizi ya mashapo ya mgodi huo.

“Baada ya ukaguzi uliofanywa Julai 12 na kurudiwa tena Julai 30 na 31, tume imeridhia tuendelee na usafirishaji dhahabu,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Acacia.

Katibu mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alithibitisha kutolewa kwa kibali hicho ili kampuni hiyo iendelee na biashara yake.

“Tumewaruhusu waendelee. Wataamua wao lini wataanza kusafirisha dhahabu nje ya nchi,” alisema Profesa Manya.

Zuio la makinikia

Mwaka 2017, Serikali iliizuia kampuni hiyo kusafirisha mchanga wa madini na mpaka leo zuio hilo linaendelea huku pande husika zikiwa na mazungumzo ya mara kwa mara kutafuta mwafaka.

Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, takwimu zinaonyesha Acacia ina zaidi ya wakia 185,800 za dhahabu; wakia 158,900 za fedha na ratili 12.1 za shaba. Makinikia hayo yote, yana thamani ya Dola 247 milioni za Marekani.

Kwa mwezi mmoja wa kuzuiwa kusafirisha dhahabu, chanzo cha kuaminika ndani ya kampuni hiyo kimesema kuna zaidi ya wakia 50,000 zinazosubiri kusafirishwa katika Mgodi wa North Mara.

Pamoja na hayo yote, Serikali imekataa kushirikiana na Acacia kutokana na mgogoro ulioibuka mwaka 2017 na mazungumzo yanayoendelea kufanywa ni kati yake na Barrick ambayo ni kampuni mama ya Acacia.

Kutokana na msimamo huo wa Serikali, Barrick imelazimika kuanza mchakato wa kununua asilimia 36.1 isizomiliki ndani ya Acacia kuharakisha kukamilika kwa mazungumzo hayo nili biashara iendelee.