Acacia yatekeleza agizo la Serikali kunusuru mgodi usifungwe

Friday March 15 2019

 

Dodoma. Uongozi wa kampuni ya Acacia kupitia mgodi wa North Mara umezungumza na Serikali kuelezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa kudhibiti maji yenye sumu.

Mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni wiki moja tu imepita tangu Waziri wa Madini, Doto Biteko atangaze kufunga shughuli za mgodi huo kama utashindwa kudhibiti maji ya sumu yanayotiririka kwenye makazi ya watu ifikapo Machi 30.

Tamko hilo la Serikali limeifanya kampuni ya Acacia kuchukua hatua za haraka za kudhibiti maji hayo ili kukwepa rungu la kufungiwa mgodi.

Machi 12 uongozi wa Acacia North Mara ulikutana na Biteko jijini Dodoma kwa lengo la kueleza hatua iliyofikiwa kutekeleza agizo hilo.

Akizungumza katika kikao hicho, kaimu mkurugenzi mtendaji wa Acacia, Samuel Pobee alisema tayari wameshachukua hatua za kudhibiti maji yenye sumu na hakuna tena yanayotiririka kuelekea kwenye kwa watu.

Alisema pamoja na kudhibiti maji hayo kupitia bwawa la kuhifadhia maji yenye sumu yajulikanayo kitaalam kama ‘tope sumu’ (Tailings Storage Facility- TSF), mgodi huo umeanza kujenga TSF mpya.

“Waziri tumekuja kutoa mrejesho wa utekelezaji wa agizo lako, tunafurahi kukuambia kuwa tumetekeleza na kwa sasa hakuna maji yanayotiririka,” alisema Pobee.

Kwa upande wake, Biteko alipongeza hatua iliyochukuliwa lakini akasema atajiridhisha baada ya kupata ripoti ya wataalamu watakaokwenda kuhakiki utekelezaji wa agizo lake.

Biteko alitoa agizo hilo Machi 6 alipotembelea mgodi wa North Mara na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyamongo wilayani Tarime.

Advertisement