AfDB yaipongeza Tanzania kukuza uchumi asilimia 7

Muktasari:

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipongeza  Tanzania kwa ukuaji  wa uchumi wa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi.

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipongeza  Tanzania kwa ukuaji  wa uchumi wa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokuwa kwa kasi.

Pongezi hizo zimetolea leo Mei 15 na Rais wa benki hiyo, Akinwumi Adesina muda mfupi baada ya kuonana na kufanya mazungumzo na Rais John magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam kuhusu ushirikiano kati ya benki hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa, pongezi hizo kwa  Rais Magufuli zimetolewa kufuatia dhamira yake njema na msimamo wake wa kuwapigania Watanzania.

“Amemtaka (Rais Magufuli) kuendelea na mwelekeo huo ambao umeendelea kuimarisha uchumi kwa ukuaji wa wastani wa asilimia 7 ikilinganishwa na ule wa dunia wa asilimia 3.5,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha Adesina amempongeza Rais Magufuli kwa ushirikiano mzuri na nchi jirani ikiwamo Uganda hivyo kufanikisha ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilometa 1,443 kati ya Hoima nchini Uganda na Bandari ya Tanga hapa nchini.

Mbali na hilo Rais huyo wa AfDB amesema wamezungumzia kuhusu kilimo, ambapo amesema benki hiyo ipo tayari kusaidia Tanzania kukabiliana na tatizo la masoko ya mazao yanayozalishwa katika kanda mbalimbali na kuongeza thamani yake.

Kuhusu miradi mingine ya maendeleo, amesema hivi sasa benki hiyo inafadhili miradi yenye thamani ya Sh 4.55 bilioni na kwamba hivi karibuni imeidhinisha ufadhili kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma za urefu wa kilometa 110 na uwanja wa ndege wa kimataifa Msalato.

Mbali na hilo, Adesina amepongeza pia ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa kutumia fedha zake na ameahidi kuunga mkono mradi hasa wa ujenzi wa kuanzia Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda, Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa upande wake, Rais Magufuli amemshukuru Adesina na kuongeza kuwa pamoja na miradi mingine, AfDB imekubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya Mpanda Tabora yenye urefu wa Kilometa 359.

“Imekubali pia kujenga awamu ya pili ya mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kati ya Kariakoo na Mbagala jijini Dar es Salaam,” amesema.

Kuhusu benki hiyo kusaidia ujenzi wa reli ya kati kwa kipande cha kuanzia Isaka  mpaka Kigali, amesema itasaidia kuharakisha usafirishaji katika Kanda ya Kati na Magharibi.