UCHOKOZI WA EDO: Afadhali tumesafisha ‘reception’ ya nchi yetu

Wednesday August 7 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Niliwahi kuandika hapa. Jinsi nilivyokuwa hodari wa kulitetea taifa pale uwanja wa ndege wa zamani, kabla ya huu mpya. Huwa nasafiri mara nyingi, wakati nikiwa narudi nchini naungana na abiria wa ndege yangu na ndege nyingine kukabiliana na karaha za uwanja ule.

Tunapanga foleni kuelekea kwa maofisa wa uhamiaji. Joto kali, ukumbi uliofurika, vyoo vya kawaida. Kulikuwa na karaha nyingi pale. Kitu cha msingi nilichokuwa nafanya ni kuwapoza abiria wa kigeni ambao sura zao zilionekana kuchanganyikiwa.

Niliishia kuwaambia ‘Shida Itaisha tu hii, wakati wa kutua hamjaona uwanja mpya? Upo hapo kando utafunguliwa muda si mrefu’. Hii ndio kazi niliyojipa kuficha aibu ya Taifa. Huu ndio uzalendo wa kweli. Wakati mwingine ama unalazimika kusema hivyo au kudanganya kitu kwa ajili ya kutetea aibu ya Taifa.

Mama mmoja wa kizungu kutoka Marekani niliwahi kumkuta katika karaha nzito ya joto. Alikuwa ameshuka na Ndege ya Emirates. Niliamua kumsaidia mabegi yake kwa upendo mkubwa. Mwishowe akaniuliza ‘Hivi hauwezi kutumia boti kufika Tanzania?” Nilijua alichokuwa anamaanisha, nikajifanya nipo bize na mizigo yake.

Mgeni ambaye angekuja kutembelea Mlima Kilimanjaro au kwenda Zanzibar, halafu kwanza akafikia Dar e salaam, asingeamini kama yupo katika nchi yenye Mlima Kilimanjaro na Kisiwa cha Zanzibar. Asingeamini kama amekanyanga ardhi ya nchi ambayo ina mbuga za Serengeti na nyinginezo.

Hatimaye wiki iliyopita Namba Moja amefungua uwanja mpya wa ndege uliokuwa unasubiriwa kwa hamu. Kwa sasa nitakuwa napita pale nikitembea kifua mbele. Ni uwanja ambao hauwezi kufanana na viwanja kama vya Dubai, Hong Kong, Madrid, Amsterdam, JF Kennedy na vinginevyo lakini walau abiria wanaweza kupumua. Walau pia utanipunguzia maneno mengi ya ujanja ujanja niliyokuwa nayaleta kwa abiria wa kigeni wakati tunawasili kutoka nje ya nchi.

Advertisement

Acha watalii na abiria wengine wakutane na matatizo wakati wameshaingia nchini, lakini kukutana na matatizo ukiwa uwanja wa ndege lilikuwa tatizo la msingi. Ni kama ndoa tu, wakati mwingine matatizo makubwa ya ndoa unayafahamu wakati umeyaingia.

Advertisement