Afisa usalama feki awaponza viongozi wa mgodi wa dhahabu

Wednesday April 24 2019Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel

Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel 

By Rehema Matowo,Mwananchi [email protected]

Geita. Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel ameagiza kukamatwa kwa katibu wa mgodi wa Nyarugusu ,Stanslaus Masunga na Tugwa Kishengena wanaotuhumiwa kufadhili fedha na kumtafuta afisa usalama wa Taifa feki ili awasaidie mgodi huo ufunguliwe.

Mgodi wa Nyarugusu ulifungwa Oktoba mwaka jana kwa kosa la kutorosha dhahabu kilo 5.72 na kuisababishia serikali hasara.

Akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa madini Dotto Biteko, leo Aprili 24,2019 Gabriel amesema Masunga kwa kushirikiana na wenzake walichanga Sh60 Milioni na kumlipa mtu huyo aliyejifanya ametoka Ikulu kwa Raisi.

Amesema pia viongozi hao walitumia vibaya jina la raisi ili kujipatia fedha kwa madai kuwa atawasaidia mgodi huo uliofungwa kwa wizi wa madini ufunguliwe.

 

Gabriel amesema kwa fedha walizomlipa mtu huyo amekuwa akitembelea ofisi mbalimbali za serikali kuchafua mkoa wa Geita pamoja na Wizara ya madini kwa mambo ambayo sio ya kweli.

“OCD mkamate katibu na huyo mwenzake nataka watueleze walimpataje huyo mtu wa Ikulu nani aliwaonyesha wahojiwe tujue chimbuko lake haiwezekani mtu anatumia jina la Rais kupata fedha na anachafua viongozi wengine kwa mambo ya uongo”alisema Gabriel

Waziri Biteko amesema kosa kubwa linalofanywa na wakurugenzi wa mgodi huo ni kuamini maisha ya ujanja ujanja ambayo sasa yanawagharimu.

Biteko amesema ataendelea kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu ,na serikali haipo tayari kukubali ubabaishaji .

“Nawaambia kila mtu atabeba mzigo wake, madalali feki mnaowatumia hawata wasaidia kupata haki kinyume na sheria “ amesema Biteko.

 

Advertisement