Afrika Mashariki hatarini kukubwa na kimbunga Idai

Muktasari:

  • Kuna uwezekano mkubwa eneo la Afrika Mashariki likakumbwa na kimbunga Idai na kuathiri kwa kiasi kikubwa eneo hilo.

Nairobi,Kenya. Kitengo cha utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya kimesema kimbunga Idai kilichozikumba nchi za Zimbabwe, Msumbiji na Malawi huenda athari zake zikatokea pia katika baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki.

Naibu mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa Kenya, Benard Chanzu  amesema kimbunga hicho huenda kikaathiri msimu huu wa mvua kwenye eneo hilo.

'Mara nyingi upepo unapovuma kila mahali huwa unaeleka katika eneo ambalo kutokea kimbunga lenye hewa nyepesi, upepo unapovuma unakwenda ukielekea kwenye hicho kimbunga,’’ amesema.

Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi ameelezea athari zilizosababishwa na kimbunga hicho katika nchi yake ‘janga la kibinadamu la kiwango kikubwa.”

Amesema idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Idai nchini humo huenda ikawa imefikia 1,000.

Kimbunga hicho kilipiga katika mji wa bandari wa Beira Alhamisi kikiwa na upepo wenye kasi ya hadi kilomita 177 kwa saa, lakini mashirika ya misaada yalifika katika eneo hilo Jumapili.

Serikali ya Msumbiji imesema watu 84 wamefariki na wengine takriban 100,000 wanahitaji kuokolewa kwa dharura karibu na mji wa Beira.

Picha zilizopigwa kutoka juu ya jimbo hilo zimeonyesha zaidi ya kilomita 50 za ardhi zimezikwa chini ya maji baada ya mto Buzi kuvunja kingo zake, shirika la msaada la Save The Children limesema.

Nchini Msumbiji mashirika kadhaa ya misaada yanasaidia jitihada za Serikali  kuwatafuta na kuwaokoa watu na kutoa misaada ya chakula, mtandao wa ReliefWeb umeripoti.