Afrika yatumia Dola 30 bilioni kuagiza chakula

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT), Geoffrey Kirenga (kulia) akizungumza kwenye kongamano la Jukwaa la Fikra linalojadili Kilimo na Maisha Yetu, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Licha ya Bara la Afrika kuwa na ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, lakini hutumia zaidi ya Dola 30 bilioni kuagiza chakula nje ya bara hilo.

Dar es Salaam. Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini (Sagcot), Geofrey Kirenga amesema licha ya Bara la Afrika kuwa na ardhi ya kutosha inayofaa kwa Kilimo, inatumia zaid ya Dola 30 bilioni kuagiza chakula.

Akizungumza katika Jukwaa la Fikra la Mwananchi leo Alhamis Mei 23, 2019 Jijini Dar es Salaam, Kirenga amesema asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo haitumiki.

“Asilimia 50 ya ardhi inayofaa kwa kilimo iko Tanzania, Zambia na Msumbiji. Ardhi yetu inafaa kwa kilimo, tangu kaskazini hadi kusini,” amesema Kirenga.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Sagcot, Kirenga amesema wameendeleza mazao ya mkakati ambayo ni mahindi na viazi.

“Bado mahindi yanalimwa kwa asilimia 25. Kwa Mkoa wa Iringa tumeona mkulima wa kawaida anaweza kupata tani 5-7, lakini kama akitumia mbinu za kilimo anapata kati ya tani 11 hadi 15 kwa hekta moja,” amesema.

Huku akitaja vikundi vya wakulima, Kirenga mesema katika Mkoa wa Njombe wapo wakulima wanaouza viazi nje ya nchi.

Na amesema katika kuboresha kilimo, wakulima hao wamefanikiwa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora.