Aga Khan, Muhimbili wawafanyia upasuaji wanawake, watoto 32

Tuesday August 13 2019

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wanawake na watoto 32 waliopata makovu kutokana na ajali wamefanyiwa upasuaji wa ngozi na sehemu zilizokakamaa ili kuwarejeshea mwonekano wao wa awali.

Ajali hiyo ni za  barabarani, moto na ukatili wa majumbani.

Mbali na wanawake hao, mmoja wa wagonjwa aliyekuwa na matiti makubwa yaliyomfanya kuwa na mwonekano mbaya, naye amefanyiwa upasuaji kupunguza ukubwa wa matiti hayo.

Akizungumza leo Jumanne Agosti 13, 2019 mkuu  wa idara ya masoko na mawasiliano wa taasisi ya utoaji huduma za afya wa Aga Khan Tanzania, Aloyce Lotha amesema mpaka upasuaji huo unaomalizika kesho wanawake na watoto 56 watakuwa wamefikiwa.

Amesema upasuaji huo unafanywa kwa pamoja kati ya Hospitali ya Aga Khan, Muhimbili (MNH) na Reconstructing Women International.

“Zaidi ya madaktari bingwa 16 wakiwemo 11  kutoka Marekani, Canada na Ulaya wanaendelea kufanya upasuaji huu muhimu, kwa hiyo wagonjwa wanaendelea kuhudumiwa na kesho tutamaliza jambo hili,” amesema Lotha.

Advertisement

Akizungumzia upasuaji wa matiti, daktari bingwa wa upasuaji wa Aga Khan,  Aidan Njau amesema wapo wanawake wanaopata maumivu wa migongo na kupoteza mwonekano wao kwa sababu ya ukubwa wa maumbile hayo.

“Kazi ya kurejesha maumbile sio rahisi kwa sababu kabla ya kufanya upasuaji huu lazima umsikilize mgonjwa ujue na upasuaji wake unachukua muda kidogo,” amesema.

Daktari bingwa kutoka Reconstructing Women International, Andea Pusic amesema upasuaji huo unaondoa unyanyapaa kwenye jamii kwa sababu wahanga wengi walijificha kutokana na hali waliyokuwa nayo.

Advertisement