Agizo la Serikali kicheko kwa wavuvi Feri

Thursday January 17 2019

 

By Jackline Masinde, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Unaweza kusema uamuzi wa Serikali kuwafutia makosa wavuvi wote walioshtakiwa kwa kutokuwa na leseni za uvuvi umerejesha hali shwari katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, jijini Dar es Salaam.

Hali hiyo inatokana na wavuvi hao leo Alhamisi Januari 17, 2019 kuonekana wakiendelea na shughuli za uvuvi tofauti na ilivyokuwa jana mchana na juzi.

Juzi, wavuvi na wauza samaki walisema Serikali inahusika na kuadimika kwa samaki katika soko hilo baada ya kuanzisha operesheni ya ukaguzi wa leseni za uvuvi, lakini jana jioni Naibu Waziri wa  Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega aliagiza  wavuvi waendelee kukatiwa leseni hadi Januari 31, 2019.

Aliwataka maofisa wa wizara na halmashauri waanze kuwafuata kwenye mialo ili kuwakatia leseni kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza leo makamu mwenyekiti wa chama cha wavuvi Mkoa wa Dar es Salaam, Salehe Msean amesema wavuvi waliokamatwa juzi, jana na leo wameachiwa wakiwemo saba wa soko hilo.

Amesema baada ya kuachiwa walianza shughuli zao za uvuvi hali iliyochangia upatikanaji wa samaki.

"Hali imerudi kawaida na samaki sasa wanapatikana si kama jana na juzi na wavuvi wameanza kuingia baharini kuendelea na shughuli zao, ukataji wa leseni unaendelea hapa feri,” amesema.

Salim Jumaa amesema wavuvi walioachiwa wamefurahishwa na agizo la  Ulega na kwamba tangu jana alasiri walianza kuvua.

Mmoja wa wanunuzi wa samaki sokoni hapo,  Mwajuma Said amesema ,"Samaki wapo ni pesa yako tu  nimefika asubuhi hapa sokoni samaki wapo na bei ni ya kawaida.”


Advertisement