Aishi na maiti ya mamake nyumbani miaka mitatu

Texas. Marekani. Mwanamke mmoja jimboni Texas nchini Marekani amekamatwa baada ya masalio ya maiti ya mamake inayooza kugunduliwa nyumbani kwake.

BBC inaripoti kwamba polisi wanaamini mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 71 alianguka mwaka 2016 na binti yake mwenye umri wa miaka 47 alishindwa kumhudumia vizuri mamake aliyefariki "siku chache baadaye" kutokana na athari ya kuanguka huko.

Masalia ya mwili wa marehemu yalipatikana kwenye sakafu ya chumba kimoja huku binti yake na mjukuu wake marehemu wakilala katika chumba cha pili katika nyumba hiyo.

Mjukuu wa marehemu alikuwa na miaka 15 wakati akiishi na maiti ya bibi yake. Na kutokana na hilo, mamake ameshtakiwa kwa 'kumdhuru mtoto' wa chini ya miaka 15.

Mjukuu huyo sasa anatazamwa na jamaa zao na anapokea msaada kutoka kitengo cha kuwalinda watoto.

Huenda mamake akakabiliwa na hadi miaka 20 gerezani na faini ya hadi $10,000.