Ajali magari ya Serikali zilivyosababisha vifo 37, majeruhi 90

Tuesday November 6 2018

 

Dar es Salaam. Ikilinganishwa na miaka mingine ya karibuni, ajali za magari ya Serikali mwaka 2018 zimeonyesha kutishia zaidi maisha ya watumishi, huku zikiacha yatima, wajane na majeruhi.

Jumla ya ajali 10 zimeripotiwa mwaka huu ambazo zilisababisha vifo vya watu 37 ambapo 20 ni watumishi wa Serikali na kujeruhi 90.

Kutokana na mfululizo wa ajali hizo, Mwananchi imechambua na kuja na idadi ya ajali za magari hayo zilizoripotiwa na kuchapishwa na magazeti yake katika kipindi cha Machi hadi Novemba mwaka huu.

Ajali zilizoorodheshwa ni zile tu zilizoleta madhara ya moja kwa moja na kuripotiwa na vyombo vya habari, ikiwemo ile iliyohusisha vijana 11 wa jeshi la kujenga Taifa (JKT) na mtumishi mmoja wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) huku vijana 50 wakijeruhiwa.

Machi 29, 2018, Wabunge sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walipata ajali ya gari wakiwa mkoani Morogoro wakitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilitokea saa 2 usiku katika barabara kuu ya Morogoro-Dodoma eneo la Bwawani, wabunge hao walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Wabunge hao ambao wote ni kutoka Zanzibar ni Haji Ameir Haji (Makunduchi), Khamis Ali Vuai (Mkwajuni), Bhagwanji Maganlal Meisuria (Chwaka), Makame Mashaka Foum (Kijini), Juma Othman Hija (Tumbatu).

Mei 21, 2018, maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) walifariki dunia katika  ajali ya gari eneo la Mtelela Barabara ya Msolwa Chalinze mkoani Pwani, wakiwa njiani kuelekea jijini Dodoma.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Saidi Amiri Moshi (Kaimu Mkurugenzi wa utafiti), Zacharia Kingu (Kaimu Mkurugenzi wa Corporate Affairs) na Martin Masalu (Meneja Utafiti).

Ajali hiyo ilihusisha gari ya serikali STK 5923 Toyota Land Cruiser lililogongana na Scania T620 AQV. Waliojeruhiwa ni Godfrey Kilolo (Meneja wa Sheria) na dereva wa gari hilo.

Juni 10, 2018, madiwani 11 walijeruhiwa katika ajali ya msafara wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James, huku mmoja kati yao akifariki dunia.

Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Kisesa kilichopo mpakani mwa wilaya ya Meatu na Itilima, baada ya gari la polisi lililokuwa kwenye msafara huo kuchomoka tairi.

Juni 14, 2018, vijana 11 wa JKT walifariki dunia katika ajali ya basi iliyotokea mkoani Mbeya.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la mteremko wa Igodima nje kidogo ya Jiji la Mbeya, pia ilisababisha kifo cha askari JWTZ na dereva, hivyo kufanya jumla ya waliokufa kuwa 13.

Mkuu wa kitengo cha dharura cha Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Prosper Bashaka alithibitisha kupokea miili ya watu 13 na majeruhi 50 wa ajali hiyo.

Julai 14, 2018, Diwani wa Kata ya Manuzi, Elias Shukia na dereva wa halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Haruna Ngata walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka mkoani Dodoma, kupasuka tairi na kupinduka mara tatu.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Mkiwa, wilayani Singida. Katika ajali hiyo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Piuz Machungwa na watu wengine wanne walijeruhiwa.

Julai 29, 2018, Watu wawili akiwamo Ofisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Shadrack Sagati na Semeni Kibiriti (36) walifariki dunia, huku watumishi wengine wanne wa wizara hiyo wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari namba STK 9565 Toyota Land Cruiser V8 wakati dereva wake alipomkwepa mpita njia, Happiness James (7), aliyekatiza barabarani ghafla, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.


Advertisement